Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chongolo azuia majungu vikao CCM 

8fdefcfddece0afcaf8322e35a8e4373.jpeg Chongolo azuia majungu vikao CCM 

Thu, 15 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza wanachama wasikilizwe, kero za wananchi zipate majibu na lazima vikao vya chama hicho viwe na ajenda za maendeleo badala ya majungu au kujadili watu.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alitoa agizo hilo alipozungumza na viongozi na watendaji wa chama na serikali wakati wa majumuisho ya ziara mkoani Mbeya.

Chongolo alisema utulivu na uimara wa chama hicho ni matokeo ya kuwaletea maendeleo wananchi, kuwa wasikivu kwao na kuheshimu misingi ya haki, amani, umoja na utulivu.

“Chama lazima kiwe kinafanya vikao na kuhakikisha vinakuwa vyenye agenda za maendeleo na sio kujadili watu, majungu au kuendeleza siasa za makundi, wakati huo huo tukumbuke wanachi wetu,” alisema Chongolo.

Alisema si uungwana wananchi kupata majibu ya kero wakati viongozi wa kitaifa wanapowatembelea na haki yao na wajibu wa lazima kwa waliopewa dhamana kufanya hivyo.

Alionya kuwa wakati CCM ikijiandaa kwa uchaguzi wa ndani si vyema wanachama kutengenezewa tuhuma za kupika ili wakose sifa za kuomba uongozi.

“CCM imeendelea kubaki kuwa tumaini pekee la Watanzania ikiwa ni matokeo ya chama chetu kujisahihisha na kurejesha imani kubwa kwa wananchi kwa kuisimamia serikali kwa ufanisi mkubwa katika kuboresha huduma za kijamii, upatikanaji wa haki, kudhibiti vitendo vya wizi, rushwa, ufisadi, kukemea vikali matumizi mabaya ya madaraka, ulinzi wa rasilimali za nchi, kuukabili utendaji kazi wa mazoea na matumizi yenye tija kwa mapato ya serikali,” alisema Katibu Mkuu wa CCM.

Alisema utulivu na uimara wa CCM umetokana na kuimarika demokrasia ndani ya chama hicho hivyo viongozi na wanachama wanapaswa kudumisha hilo.

Chongolo alitaja sababu nyingine inayoongeza imani ya CCM na kukubalika kwake kwa umma ni kuimarika demokrasia, kutoweka makundi, uadilifu na uwajibikaji kupewa msukumo.

“CCM ndio tumepewa dhamana ya kutoa uongozi wa nchi yetu na kuunda serikali hivyo tusikubali mambo ya hovyo yakafanyika chini ya dhamana hii tuliyopewa,” alisema.

Chongolo na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wamehitimisha ziara katika mikoa ya Rukwa, Songwe na Mbeya.

Chanzo: www.habarileo.co.tz