Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chongolo ataka shule 200 za kata ziwe za kilimo

2112fec4653b630eac4a00477415aac8.PNG Chongolo ataka shule 200 za kata ziwe za kilimo

Fri, 12 Aug 2022 Chanzo: Habari Leo

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitawasiliana na kumshauri Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ili shule mpya 200 za kata zinazojengwa nchini kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), ziwe na mchepuo wa kilimo.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, lengo ni kupata wataaluma ya sayansi ya udongo watakaosaidia jamii katika kilimo chenye tija.

Chongolo alisema hayo jana alipokagua ujenzi wa shule ya Kata ya Kisiwani ambayo ametoa maelekezo iitwe Shule ya Sekondari Manofu, kuenzi mwananchi wa Amani aliyetoa ekari zake tatu kwa ujenzi wa shule hiyo baada ya eneo la kujengwa shule kukosekana.

Alisema serikali imedhamiria kuboresha kilimo, na hilo linaonekana kupitia bajeti ya Wizara ya Kilimo ambayo imeongezeka kwa kiwango kikubwa huku pia bajeti ya ruzuku ya mbolea ya Sh bilioni 300 ikitolewa, lengo ni wakulima wapate pembejeo na kulima kwa tija.

Alisema katika ujenzi wa shule mpya 200 za kata nchini unaoendelea, umefanywa kuzingatia ubora wa elimu na kujengwa maabara za kisasa za kutosha hivyo ili kuboresha kilimo, atawasiliana na kumshauri Profesa Mkenda shule hizo ziwe na mchepuo wa kilimo.

“Nitazungumza na Waziri wa Elimu ili shule mpya za sekondari za nchini zile 200 zinazojengwa kupitia Mradi wa SEQUIP ziwe na mchepuo wa kilimo kwa kuwa zina maabara za kutosha wanafunzi wetu wasome sayansi ya udongo, wajifunze uzalishaji wa mazao wenye tija na kusaidia jamii zetu,” alisema Chongolo.

Alisema serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imetoa Sh bilioni 100.58 kujenga shule za sekondari mpya 214 za kata katika majimbo yote yasiyo na shule za sekondari za kata nchini.

Akizungumzia ujenzi wa shule mpya ya Kata ya Kisiwani aliyoagiza iitwe Manofu, aliagiza kumegwa ardhi katika Hifadhi ya Msitu wa Amani ili kupanua ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Kisiwani.

Amewaagiza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omar Mgumba na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Halima Bulembo, kukaa na Meneja wa Wakala ya Misitu Tanzania (TFS) mkoani humo kuandika barua kwenda kwa Mtendaji Mkuu wa wakala hiyo kuomba kumegewa ardhi hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa wa Jimbo la Muheza, Hamisi Mwinjuma, kusema shule hiyo haina eneo na eneo ambao shule imejengwa, ni ekari tatu ambazo ni ndogo zilizotolewa na mwananchi.

“Shule hii ikikamilika iko katika mazingira rafiki ya kusoma sasa ni vyema tuendeleze majengo ya kidato cha tano na sita na hapa mmesema eneo ni dogo. Kwanza hii shule iitwe Manofu kuthamini mwananchi aliyetoa ardhi yake kujenga shule,” aliagiza Chongolo.

Awali, akisoma taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, Msimamizi wa mradi huo, Toge Buhimila alisema utekelezaji wake unafanywa kwa gharama ya Sh milioni 470 ambazo ni fedha kupitia SEQUIP.

Alisema ujenzi wa mradi ulioanza Machi mwaka huu na utakamilika Septemba 20, mwaka huu, umejenga vyumba nane vya madarasa, maabara tatu, jengo la utawala, maktaba na la Tehama pamoja na matundu 20 ya vyoo.

Awali akizungumzia ujenzi wa shule hiyo, mbunge Mwinjuma maarufu Mwana FA, alisema shule hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano wa wananchi kupitia ‘force account’ ambapo wananchi wamechangia nguvukazi ya zaidi ya Sh milioni 17 ili watoto wao wanaotembea kilometa 23 kila siku kufuata shule kata za jirani, wapate shule jirani.

Hata hivyo, Chongolo pamoja na mambo mengine, alisema amechukua ombi la shule hiyo kuongezewa Sh milioni 130 ili kukamilisha ujenzi wake na kupanua majengo ya kidato cha tano na sita na kuahidi kwenda kulifanyia kazi ili fedha hizo zipatikane.

Chanzo: Habari Leo