Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakuna chama chochote cha siasa chenye milki wala agenda ya Sensa ya watu na makazi na kuwataka wananchi wote kujitokeza kuhesabiwa kikamilifu kwa manufaa yao.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu CCM, Daniel Chongolo katika Kata ya Kilulu wilayani Muheza mkoani Tanga, alipokagua uhai wa chama hicho ngazi ya mashina ,katika Shina namba tatu.
Akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani, Chongolo amesema hakuna chama chochote cha siasa nchini ambacho Sensa ya Watu na Makazi ni agenda yao, hivyo wasikubali kuhadaiwa kwenye hilo.
"Niwaambie hatuna chama chochote cha siasa nchini iwe CCM wala chama kingine wala taasisi itasema sensa ya watu na makazi ni agenda yao, msikubali sensa kuingizwa siasa, sensa ni kwa maendeleo yenu na sio ya serikali,"amesema Chongolo.
Amesema Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanywa Agosti 23,mwaka huu ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wenyewe na kuwataka wananchi wajitokeze kuhesabiwa, ili serikali ijue idadi yao iweze kupanga vizuri bajeti kulingana na wingi wa watu katika maeneo yao.
"Tunahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha, tunafanya hivi sio kwa ajili ya CCM au chama kingine, bali ni kwa ajili ya maendeleo yenu, msipojitokeza kuhesabiwa ni hasara kwenu, hivyo msikubali kudanganywa mkihesabiwa nyie ndio mnanufaika pindi serikali inapotaka kupanga bajeti ya maendeleo kwenye maeneo yenu,"amesisitiza Chongolo.