Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amemkingia kifua mkandarasi anayejenga mradi wa maji Katumba, Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa asichukuliwe hatua kwa makosa ya viongozi wa Serikali.
Mkandarasi huyo ni Posh alliance Limited and Sibika Trade & Construction Ltd Joint Venture ya Dar es Salaam wanatekeleza mradi huo kwa gharama za Sh2.53 bilioni.
Chongolo amefikia uamuzi huo leo Jumatano, Oktoba 11, 2013 alipofika kukagua mradi huo na kupokea taarifa kutoka kwa Mathew William akimwakilisha Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Sumbawanga.
William amesema mradi huo umefikia asilimia 27.4 na mkandarasi amelipwa Sh379.7 milioni ambazo ni malipo ya awali huku malipo mengine Sh743.46 milioni zikichelewa kulipwa.
Amebainisha malipo hayo kuchelewa ni miongoni mwa changamoto. Hata hivyo, wamempa barua ya onyo mkandarasi huyo zinazohusu kuzingatia muda wa utekelezaji.
Amesema wamekubaliana kusitisha mkataba baina ya mwajiri na mkandarasi kuanzia Oktoba 2, 2023 kwa faida ya pande zote.
Baada ya taarifa hiyo, Chongolo amesema wanasitishaje mkataba wakati mkandarasi hajalipwa malipo yake huku akisema fedha zimetolewa ili kutekeleza mradi huo lakini waliopewa dhamana wameshindwa kuzitoa.