Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chongolo amjengea nyumba Balozi wa Shina

Balozi Pic Chongolo amjengea nyumba Balozi wa Shina

Tue, 30 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya balozi wa Shina namba Saba, Tawi la Ilambilole, Jimbo la Isimani, Rose Nyembela.

Harambee hiyo imefanyika katika nyumba ya Balozi Rose, wakati wa kikao cha Shina alichoongoza.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi alisema kikao cha Chongolo kwenye shina hilo kimesaidia kupaisha sauti ya Rose ambayo haikuwa rahisi kusikika.

"Niseme tu mimi ni mkongwe wa siasa lakini sikumbuki lini nimekaa kikao kama ulivyokaa Katibu Mkuu, imesababisha sauti ya mama huyu mnyonge, anayeishi mazingira haya magumu tena katika nyumba ya kupanga kusikika," amesema Lukuvi.

Kauli hiyo ya Lukuvi ilimuinua Sophia Mjema, Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi kuanzisha mchakato huo ili kumjengea balozi huyo nyumba bora.

"Hapa kuna viongozi wengi Wanawake tuanze sisi tumsaidie mwenzetu, sisi tuanze kuchangia ujenzi wa nyumba hii," amesema Mjema.

Tayari mama huyo ameshapokea fedha kwa ajili ya kiwanja, fundi, matofali, mawe,madirisha, milango, mbao, rangj na bati 100.

Chongolo amesema mwezi mmoja na nusu ujao, nyumba hiyo itakuwa imekamilika na kufanyiwa uzinduzi.

Kiongozi huyo wa CCM, Chongolo amesema chama hicho kipo ngazi ya shina ndio maana viongozi hao wameshuka huko kwa ajili ya kuendeleza uhai.

Hata hivyo amesema safari ijayo, wataanza kushindanisha mabalozi na anayefanya vizuri kikao kitafanyika kwake na hawatamuacha kama walivyo mkuta.

Balozi Rose alishukuru kwa msaada huo wa nyumba na kwamba, imempa ari kubwa zaidi kuendelea kukipigania chama hicho.

"Nashukuru sana, kweli nyumba hii nilipanga lakini CCM inanipatia nyumba. Asante Sana," amesema Rose ambaye alikuwa amepiga magoti kuonyesha shukrani.

Katika harambee hiyo, Katibu Mkuu Chongolo ametoa tofari zote, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yassin ametoa madirisha na milango, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Mkoa wa Iringa mifuko 100 ya simenti na misumari, Mnec Leonard Mahenda mbao na Mnec Richard Kasesera Mawe.

Katibu wa Oganaizesheni ya CCM, Issa Haji Gavu amechangia gharama za ufundi na wengine waliochangia ni Mwenyekiti wa UWT, Mkoa wa Iringa, Zainab Mwamwindi, Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa, Fatma Rembo na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa huo, Seki Kasuga na Dickson Mwipopo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live