Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chongolo akemea wanaotolea macho uchaguzi mkuu 2025

55541ca41837142dc90deeef6f776eec Daniel Chongolo, Katibu Mkuu CCM

Mon, 11 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amekemea wanachama wa chama hicho wanaotolea macho Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 na kuwataka kuelekeza nguvu zao katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho utakaofanyika mwaka huu.

Amesema kumezuka tabia ya baadhi ya wanachama kufikiria zaidi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuota ubunge na udiwani na kusema tabia hiyo inazorotesha shughuli za chama.

"Mwanasiasa mzuri ni yule anayehangaika siku ikifika, anahangaika na jambo wakati muafaka, anahangaika na uchaguzi huu wa ndani, acheni kupanga safu, acheni kutengeneza watu," alisema Chongolo.

Katibu Mkuu huyo wa CCM alisema kila mwana CCM ana haki ya kugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho na kusisitiza hakuna mwanachama mwenye hati miliki wa nafasi yoyote.

"Ni haki ya kila mmoja kujitokeza na kutimiza wajibu wa kikatiba kugombea nafasi yoyote, usitishwe, usiogopeshwe, usibabaishwe, jipime usiogope chochote sote tuna haki sawa katika uchaguzi hakuna aliye zaidi ya mwingine," alisema.

Alisema kwa kipindi kifupi akiwa katika mkutano huo amepokea meseji zaidi ya 800 za watu kufanyiana fitina, jambo alilosema ni nongwa na halisaidii.

"Tumepita mwaka 2010, tumeenda 2015, leo unakuja kumuhukumu mtu kwa mambo ya 2010, huo ni uchawiuchawi, acheni nongwa, acheni watu watumie haki zao za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi kugombea nafasi mbalimbali," alisisitiza.

Chongolo aliwataka wanachama wa CCM wakiwemo wanawake na vijana kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdurhaman Kinana mbali na kumpongeza Chongolo, aliwataka wana CCM kuwapa zaidi nafasi vijana na wanawake katika kuwania nafasi hizo kwa kuwa wakati mwingine ni ngumu kwao kupenya kwa sababu mbalimbali.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba alisema kuna ushirikiano mzuri baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali na hiyo ni kutokana na uwapo wa wabunge, mameya na madiwani wengi wanaotokana na chama hicho.

Aliwataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa matawi na mashina ili chama kiweze kupata mtaji mkubwa wa wanachama .

Chanzo: www.tanzaniaweb.live