Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chongolo ainyooshea kidole UWT “mmeanza kujisahau”

Chongolo Dan Chongolo ainyooshea kidole UWT “mmeanza kujisahau”

Mon, 28 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema Jumuiya ya Wanawake ya chama hicho (UWT) imeanza kujisahau kwa kuacha kuwa viongozi wa jumuiya na chama na badala yake kuwa viongozi wa watu.

 Chongolo ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 28, 2022 wakati wa uchaguzi wa viongozi wa umoja huo.

Amesema jumuiya hiyo ina nguvu sana lakini nafikiri kuna mahali kuna kujisahau kwa kutokaa katika nafasi zao.

“Kuna mahali tunaanza kujisahau, tunaacha kuwa viongozi wa jumuiya ya wanawake, viongozi wa jumuiya na chama tunakuwa viongozi wa watu. Hilo jambo linatengeneza changamoto kubwa ya uimara wa UWT na nguzo muhimu ya wanawake,” amesema.

Amesema ni lazima kutambua chama ni kikubwa kuliko mtu yoyote na kwamba ni lazima wasimame katika nafasi zao na kurudi kwenye misingi ya chama ya chama chao.

Amewataka wafahamu chama kwanza watu baadaye.

Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana amewataka wanawake hao kushikamana na kuwa kitu kimoja wakati wote kwasababu nguvu ya chama chao ni umoja na mshikamano.

“Jumuiya ya wanawake inatarajia kuwa jumuiya ambayo inatetea maslahi makubwa na mpana ya wanawake wote nchini. Ni muhimu mkaelewa sera za chama chetu mtakaochaguliwa,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu wa umoja huo, Dk Philis Nyimbi alisema idadi ya wajumbe wote waliowa wakitakiwa ni 830 lakini waliokuwa ukumbini walikuwa 802 hivyo akidi iliyotakiwa ilikuwa imefikiwa.

Viongozi waliohudhuria ni pamoja na viongozi wastaafu Makamu wa CCM Bara, Philip Mangula, Mwenyekiti mstaafu wa UWT, Sophia Simba na Spika mstaafu Anne Makinda.

Wengine ni wawakilishi wa vyama vya siasa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Frelimo (Msumbiji), Zanu PF (Zimbabwe) na ANC (Afrika Kusini).

Wagombea waliopitishwa na Halmashauri Kuu ni, Gaudentia Kabaka (anayetetea nafasi yake), Kate Kamba, Dk Wemael Chamshama, Mariam Lulinda na Mary Chatanda huku mchuano mkali ukionekana kwa Gaudentia Kabaka, Kamba na Mary Chatanda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live