Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chongolo aiagiza serikali ujenzi wa madarasa  

6c4f7b4f7e7a4baeda536c2eef6f74da.jpeg Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo

Thu, 12 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameiagiza serikali itenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa ya shule kwa ajili ya mwezi Januari, mwakani.

Katibu Mkuu huyo wa CCM alitoa agizo jana Agosti 11, wakati akiwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi na shughuli za maendeleo mkoani Dar es Salaam.

"Nitumie fursa hii pia kutoa maagizo mahususi kwenye eneo la elimu, kama nchi tumekuwa na changamoto kubwa sana ya kufanya baadhi ya mambo kwa zimamoto, kila mwaka tumekuwa tukisubiria mwezi Desemba kuhangaika kukimbizana na madarasa kama vile ni jambo la dharura kama vile hatujui maoteo kwa kipindi cha mwaka mzima,na hatujui bajeti nzima,” alisema.

Alisema serikali inatenga fedha kila mwanzo wa mwaka wa fedha Julai Mosi kwa ajili ya kutumika kwenye miradi ukiwamo ujenzi wa madarasa.

"Sasa mwaka huu lazima robo hii ya mwaka itumike kutenga fedha zote ambazo zipo kwenye bajeti kuzielekeza kutumika kwenye miradi ya miundombinu ya madarasa ya shule zetu ili ikifika Januari, 2022 watoto wetu wote wapokelewe kwenye shule zetu bila usumbufu wala kufanya mambo kwa dharura, lazima tusimamie haya mambo ili tutafsiri matokeo yenyetija ya elimu bila malipo," alisema.

Katika ziara hiyo, Chongolo alitembelea mradi wa Daraja la Tanzanite awali likifahamika kama Daraja la Salenda na mradi wa ujenzi wa soko la kisasa maeneo ya Tandale.

Alipongeza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kwa usimamizi mzuri wa mradi huo pamoja na kujumuisha wakandarasi wengi wazawa na akaagiza kuwe na programu maalumu ya kukuza wakandarasi hao.

Chanzo: www.habarileo.co.tz