Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema kwamba hakuna mtu mkubwa kuliko chama hicho na kwamba wale wote wanaokijaribu ama kushindana na chama hicho utaratibu umewekwa hivyo wangoje matokeo.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Agosti 11, 2021, Jijini Dar es Salaam, alipoulizwa kuhusu uwepo wa kauli kinzani zinazotolewa hadharani na baadhi ya wanachama wa chama hicho wakiwemo wabunge kuhusu maamuzi ya serikali kuleta chanjo ya COVID-19 nchini.
"Kuhusu kauli kinzani niseme hiki chama ni kikubwa kuliko mtu yeyote, hata mimi Katibu Mkuu sina mamlaka ya kuweka ya kwangu na kubeba agenda za kwangu, chama hiki kimeweka utaratibu hata wa kuhangaika na mimi nikianza kufanya mambo ya hovyo," amesema Chongolo.
Aidha, Chongolo ameongeza kuwa, "Chama hiki kimekuwa kinachukua hatua katika mazingira ambayo kila mmoja anapanua mdomo na kushangaa na hao unaofikiri kwamba wana uwezo wa kufikiria kushindana ama kukijaribu chama hiki, chama hiki kina utaratibu umewekwa, subiria matokeo".
Miongoni mwa wabunge waliotoa kauli hadharani kuhoji uhalali wa chanjo ya Corona kwa wakati huu na wale waliotamka kwamba hawatachanjwa ni Mbunge wa Kawe Josephat Gwajima na Mbunge wa kuteuliwa Hamphrey Polepole.