Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chekeche la uspika laiva

Uspikapic Data Chekeche la uspika laiva

Tue, 18 Jan 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wakati leo CCM inaanza mchakato wa kuwachuja makada wake 70 wanaoomba kuteuliwa kuwania nafasi ya Spika wa Bunge, mgombea mmoja wa chama cha upinzani amejitokeza kuchukua fomu.

Nafasi ya Spika wa Bunge iko wazi baada ya kujiuzulu kwa Job Ndugai aliyekuwa Spika tangu Novemba 17, 2015.

Kwa mara ya kwanza wakati Ndugai akigombea nafasi hiyo, Katibu wa Bunge alikuwa Dk Thomas Kashilillah ambaye kwa sasa naye ni miongoni mwa makada 70 waliorejesha fomu kati ya 71 waliokuwa wamezichukua kuomba ridhaa ya chama kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, hadi CCM inaanza mchakato wa kuchuja majina ya waombaji hao, ni chama kimoja cha upinzani cha ADC kimefungua pazia na mwanachama mmoja jana alijitokeza kuchukua fomu.

Mwanachama huyo, Maimuna Kassim aliyewahi kugombea ubunge jimbo la Kilindi mkoani Pwani katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, alichukua fomu jana katika ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni, Dar es Salaam.

Maimuna alikabidhiwa fomu hiyo na Kaimu naibu katibu mkuu Bara, Doni Mnyamani na gharama za fomu hizo kwa chama Sh100, 000, wakati kwa CCM ni Sh1,000,000.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM mwishoni mwa wiki, kikao cha Sekretarieti kinakaa leo kujadili wagombea hao na kuishauri Kamati Kuu ya CCM inayotarajia kukutana kesho na keshokutwa kwa ajili ya kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea.

Majina matatu yatakayoteuliwa na Kamati Kuu yatawasilishwa katika kamati ya wabunge wa CCM kati ya Januari 21, 22 au 30 kuyapigia kura kupata jina moja la mgombea wa chama hicho kwa nafasi ya Spika.

Makada wa CCM waliojitokeza sasa wamo wabunge Mussa Azzan Zungu, Dk Tulia Ackson, Luhaga Joelson Mpina, Stella Martin Manyanya, Godwin Kunambi na Joseph Musukuma.

Pia, wamo wabunge wa zamani, Stephen Masele (Shinyanga Mjini), Athuman Mfutakamba (Igalula), Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Profesa Norman Sigalla (Makete), Dk Titus Kamani (Busega), Ezekiel Maige (Masalala) na Sophia Simba (Viti Maalumu).

Kwenye kinyang’anyiro hicho kuna katibu wa Bunge wa zamani Thomas Kashilillah, pia wamo watumishi wa umma, makada, viongozi wa zamani wa Serikali na wanafunzi wawili wa vyuo vikuu.

Vyama vingine vya upinzani

Makamu mwenyekiti wa Chadema Bara, Salum Mwalimu alipoulizwa jana kwa njia ya simu kama watasimamisha mgombea katika nafasi hiyo, alisema aulizwe Katibu Mkuu, John Mnyika ambaye simu yake haikuwa inapatikana.

Siku chache baada ya Ndugai kujiuzulu, Mwalimu alipoulizwa msimamo wa Chadema kwenye nafasi ya Spika alisema suala hilo lingeelezwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu.

Katibu Mwenezi wa chama cha ACT-Wazalendo na kaimu naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salim Bimani alipoulizwa msimamo wa chama chao alisema anazungumza kwanza na katibu kkuu.

Hata hivyo, siku kadhaa zilizopita alipoulizwa kama chama hicho kitasimamisha mgombea, alisema watakutana na kutoa msimamo.

Pia, Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha Wananchi CUF na kaimu Katibu Mku, Magdalena Sakaya, alipoulizwa alisema watakapokutana watatoa msimamo.

Sakaya akizungumza na gazeti hili jana alisema walikutana lakini hawakufikia mwafaka na leo wanatarajia kukutana tena kuzungumzia suala hilo.

Chadema imewahi kusimamisha wagombea wa nafasi ya Spika mara mbili, Novemba 10, 2010 ilimteua Mabere Marando kugombea nafasi akishindana na mgombea wa CCM, Anne Makinda.

Makinda aliteuliwa na CCM baada ya kuwashinda wenzake kwenye kamati ya wabunge wa CCM kwa kupata kura 211.

Kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya Spika kwenye Bunge la 11 ndani ya CCM kulikuwa na makada zaidi ya 22 waliowania kuteuliwa na chama chao kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, kamati ya wabunge wa CCM ilimchagua Ndugai kugombea nafasi ya Spika na Dk Tulia nafasi ya Naibu Spika.

Kwenye nafasi ya Spika, vyama vya upinzani saba viliwasilisha majina ya wagombea wao.

Ndugai alipata ushindani kutoka kwa wagombea wengine saba kutoka upinzani, lakini mpinzani wake wa karibu alikuwa mgombea wa Chadema, Goodluck Ole Medeye aliyepata kura 109 dhidi ya kura 264 sawa na asilimia 70, zilizompa ushindi.

Ole Medeye amejitokeza tena kuwania nafasi hiyo, safari hii akiomba kupitia CCM.

Wagombea wa upinzani waliojitokeza kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la 11 walikuwa Peter Sarungi (AFP), Hassan Almas (NRA), Dk Godfrey Malisa kutoka (CCK), Goodluck Ole Medeye (Chadema), Richard Lyimo (TLP), Hashim Spunda Rungwe (Chaumma) na Robert Kasinini (DP).

Chanzo: www.mwananchi.co.tz