Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chaumma wachagua viongozi wapya, Rungwe ajisifia

50844 Pic+chauma

Sun, 7 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Umma (Chaumma) leo Jumamosi Aprili 6, 2019 kinafanya uchaguzi wake wa viongozi wa kitaifa huku mwenyekiti wake, Hashim Rungwe akitetea nafasi yake.

Uchaguzi huo ni wa pili kufanyika tangu chama hicho kilipoanzishwa mwaka 2012. Uchaguzi mkuu wa kwanza ulifanyika mwaka 2014 jijini Dodoma na Rungwe akachaguliwa kuwa mwenyekiti kwa kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mwenyekiti Rungwe amesema katika kipindi cha uongozi wake, chama hicho kimepata mafanikio makubwa ikiwamo kusimamisha mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2015 kwa Tanzania na Zanzibar.

"Chama chetu kimeimarika sana na kinakubaliwa na wananchi wengi. Tukimaliza uchaguzi huu, tunaanza maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Tunaamini tutashinda vijiji na mitaa mingi," amesema Rungwe.

Kwa upande wake, makamu mwenyekiti wa Chaumma-Zanzibar, Mohammed Masoud Rashid amesema chama hicho kinatoa nafasi kwa wanawake kupata nafasi za uongozi ndani ya chama kwa sababu nao ni sehemu ya ukuaji wa chama na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Baadhi wa wajumbe wa mkutano huo wamempongeza mwenyekiti Rungwe kwa kukijenga chama tangu alipopewa dhamana hiyo mwaka 2014 na kwamba chama hicho kinahitaji kiongozi ambaye atakiwezesha kupata nafasi za uwakilishi kwenye mabaraza ya madiwani na Bunge.

"Nimefurahishwa na maandalizi ya mkutano huu, ninaamini tutapata viongozi ambao watakibeba chama kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi ujao wa mwaka 2020," amesema Zuberi Mpinde, mjumbe wa mkutano huo kutoka Lindi.

Wanaogombea nafasi ya mwenyekiti kwenye uchaguzi huo ni Abbas Hussein na Hashim Rungwe ambaye anatetea nafasi yake. Nafasi ya makamu mwenyekiti Zanzibar inagombewa na Juma Mkindwi na Mohammed Masoud Rashid anayetetea nafasi yake.

Nafasi ya makamu mwenyekiti inagombewa na Salam Abubakar na Kayumbo Kaputari ambaye anatetea nafasi yake. Katibu Mkuu anatarajiwa kuteuliwa na mwenyekiti baada ya kushauriana na viongozi wenzake.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz