Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama cha NLD chakana kauli ya mwenyekiti wake

Chama cha NLD chakana kauli ya mwenyekiti wake

Mon, 18 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Mwenyekiti wa chama cha National League For Democracy (NLD) Oscar Makaidi kutangaza chama chake kujitoa kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, katibu mkuu wa chama hicho amejitokeza na kueleza kuwa kamati kuu haitambui uamuzi huo.

Katibu Mkuu huyo Tozy Matwanga amepingana na msimamo wa  mwenyekiti wake akieleza kuwa huo ni uamuzi wake binafsi na hauna  baraka za chama hivyo chama hicho kitaendelea na mchakato wa kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Novemba 13, Mwenyekiti wa chama hicho Oscar Makaidi alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akieleza kuwa NLD imejitoa kushiriki kwenye uchaguzi huo sambamba na kumtaka Waziri wa Tamisemi Suleiman Jafo ajiudhuru kwa kuruhusu mchakato wa kuwapata wagombea kuwa na dosari.

“Kwa ujumla uchaguzi umepoteza sifa ya kuitwa uchaguzi. Kwahiyo tumeamua kujitoa, na tunamtaka Waziri mwenye dhamana ya uchaguzi huu, Selemani Jafo kujiuzulu mara moja kwa kushindwa kusimamia na kulitia taifa hasara.

Matwanga amesema Makaidi amefanya maamuzi binafsi kwa ajili ya chama bila kushirikisha kamati kuu jambo ambalo ni uvunjaji wa katiba.

Amesema kufutia hilo chama hakiutambui uamuzi huo na kitaendelea kushiriki kwenye uchaguzi huo kama kawaida na hakitaweza kujitoa kwa manufaa ya mtu mmoja.

 “Kamati kuu yote hatuna taarifa, amekurupa yeye mwenyewe kufanya uamuzi binafsi. Chama hakitambui uamuzi huo tutashiriki kama kawaida na wagombea wetu wasiyumbishwe washiriki kwenye kampeni na uchaguzi pia, Wagombea wetu wamepata gharama za maandalizi yao ya uchaguzi kwa maana hiyo chama hakiwezi kuwapuuza,”

Chanzo: mwananchi.co.tz