Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama cha AFP kumwajibisha mgombea wake

14129 Kiongozi+pic TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha AFP, Rashid Rai amesema watamchukulia hatua kali za kisheria mgombea wao aliyeshindwa kurejesha fomu katika jimbo la Korogwe Vijijini, Abdulaziz Abdallah ikiwa watajiridhisha  alirubuniwa kufanya hivyo.

Alisema utafiti wa awali walioufanya, mgombea wao kwa sababu zake binafsi alishindwa kurejesha fomu zake japo baadae alisimama kuilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ulivikutanisha vyama vya DP na Demokrasia Makini, leo Agosti 27,2018,  Rai amesema tangu vunguvungu la kuhama vyama lilipoanza kumeibuka genge la wahuni wa kisiasa ambao kwa makusudi wamekuwa wakiwarubuni wagombea ili wakache kurejesha fomu.

"Sasa hawa wagombea wetu wakikacha kurejesha fomu, chama kimoja kinapita bila kupingwa, kwa kweli hatutakubali na tunaendelea na utafiti tukijiridhisha wagombea wetu waliofanya hivyo tutawachukulia hatua kali za kisheria akiwepo wa Korogwe," amesema.

Amesema mgombea wao wa jimbo la Korogwe walishirikiana nae tangu hatua za mwanzo kwa kumtumia pesa za kulipa ada na kuapa mahakamani lakini dakika ya mwisho ya kurejesha fomu alizima simu.

"Tulipiga simu tume tukaambiwa mkurugenzi yupo ofisini maajabu mgombea wao hakutokea, hivi hamuoni ajabu kwamba madiwani 40 kati ya 70 wanapita bila kupingwa?" alisema.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya alisema kutokana na hali hiyo vyama vya siasa visivyo na wabunge bungeni vitafanya utafiti kujua sababu za maeneo mengi kupita bila kupingwa.

"Tutatoa tamko rasmi kueleza uhalisia na tuviase vyama vikubwa vifanye tafiti juu ya wagombea wao kwani badala ya kuilalamikia tume, wawachunguze hata wagombea wao," amesema

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Demokrasia Makini, Mohamed Abdulah amesema umakini katika kuchagua wagombea hasa katika chaguzi ndogo ndio utakaoweza kuleta ushindani wakweli.

Chanzo: mwananchi.co.tz