Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yawataka wananchi Ukonga wasisuse uchaguzi

14612 UKONGA+PIC TanzaniaWeb

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wananchi wa Ukonga wameombwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Septemba 16, ili wasipoteze haki zao kwa kuususia uchaguzi huo.

Hayo yalisemwa jana na diwani wa Kata ya Majohe, Waziri Malijale katika mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Ukonga, ulioandaliwa na Chadema katika viwanja vya Italian vilivyopo Buyuni, Chanika.

“Niwaambie wanaBuyuni na Ukonga kwa ujumla msisusie kwenda kupiga kura, mkifanya hivyo ni kuwapa mafanikio msiowapenda,” alisema.

Malijale aliwataka wananchi kutambua kuwa Tanzania ni nchi yao, hivyo wasikubali kudanganywa na kwamba Septemba 16 wakamuonyeshe (Mwita)Waitara kwamba aliacha ubunge mwenyewe, hivyo hakuwa na sababu ya kuomba tena kuchaguliwa.

Alisema ubunge na udiwani ni mali ya wananchi, hivyo mwenye cheo hicho hana mamlaka ya kufanya atakavyo wakati waliompa ni wananchi.

“Niwaombe wana Buyuni msisusie kwenda kupiga kura mkifanya hivyo ni kumpa mafanikio, kuna wajumbe wanazunguka mtaani kununua shahada ukiona mtu kama huyo ni mwizi mkamateni na kumfikisha eneo husika ni wizi na kosa kisheria,” alidai Malijale.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga, Asia Msangi alisema akichaguliwa kuwa mbunge kazi yake ya kwanza ni kuwaunganisha watu.

“Mimi ni mbunge nitakayewaunganisha watu, kuna makundi mengi kwenye jamii nitawaunganisha wakiwemo kinamama, kuna changamoto za kiuchumi,” alisema Msangi.

Alisema akiwa mbunge atahakikisha wanapata mikopo midogo midogo itakayowasaidia kuinua hali zao kiuchumi.

“Naomba niwaambie mama hakimbii familia, nawaambia nitapambana mpaka mwisho nawaambia msiogope tuuvae ujasiri tulipiganie taifa,” alisema Msangi.

Aliwaomba wazee wa Jimbo la Ukonga kuwa karibu naye kwa kuwa wamesahaulika kwa muda mrefu, ikiwamo kukosa huduma muhimu wanazostahili kupata bure.

Msangi alisema kwa upande wa vijana atahakikisha anaanzisha mashindano ya mpira wa miguu katika jimbo hilo, lengo ikiwa ni kuitumia fursa hiyo kuwa ajira kwa vijana.

Naye mkuu wa idara ya usalama na ukufunzi wa Chadema, Singo Kigaia alisema wakati wa uchaguzi waliyahangaikia majimbo na kupata ushindi lakini Waitara aliamua kuzipuuza juhudi hizo na kukimbilia CCM.

“Hamuwezi kuwa na kazi ya kumchagua Waitara kwenye Jimbo la Ukonga kila siku, kama aliuchoka ubunge akae pembeni aingie mwingine naye ni Asia Msangi,” alisema Kigaia.

“Waitara ameshawishiwa akapewa ahadi na kwamba mwaka 2015 CCM ilifanya kura za maoni mwaka huu kura za maoni zimefanyika? Watu wa Ukonga tuliamua miaka mitano ni ya Chadema tutaendelea kukalia kiti,” alisema Kigaia.

Chanzo: mwananchi.co.tz