Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yatoa tamko kukabiliana na corona

99745 Pic+chadema Chadema yatoa tamko kukabiliana na corona

Fri, 20 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema kimeitaka Serikali ya nchi hiyo kufunga mipaka ya nchi na kuwaweka katika karantini wageni wanaoingia nchini ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona (COVID19). 

Taarifa iliyotolewa na Waziri Kivuli wa Afya ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho, Cecilia Paresso leo Ijumaa Machi 20, 2020 imeitaka Serikali kusimamia udhibiti wa janga hili kwa umakini na weledi mkubwa.

“Serikali ihakikishe mipaka yote inafungwa ili kutoruhusu wageni na hata Watanzania waliopo nje ya nchi kwa lengo la kutoleta maambukizi mapya isipokuwa tu kwa safari na mizigo ya lazima,” amesema Paresso.

“Pale inapobidi wageni kuingia basi Serikali iwaweke kwenye karantini wageni hao kwa gharama zao kwa siku 14 kama ambavyo taratibu za kitabibu zinavyolekeza. Hii ni kwasababu wagonjwa wote waliothibitika mpaka sasa ni waliotoka nje ya nchi na si waliokuwa hapa nchini,” amesema

Licha ya Paresso kukiri kuwapo kwa athari za kufunga mipaka ya nchi ikiwa ni kuathiri utandawazi wa kibiashara na kiuchumi, lakini amesema afya na uhai wa mwanadamu hauwezi kulinganishwa na thamani ya kitu chochote.

“Ni vema kwa sasa tusiangalie na kuwaza tu faida za muda mfupi katika za utalii, biashara na uchumi kwa kuacha mipaka wazi jambo ambalo litakuja kutufanya tujute baadaye kama Taifa,” amesema huku akirejea hali ilivyo nchini Italy.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Amesema kwa kuwa mgonjwa wa virusi hivyo anatakiwa kuwa chini ya uangalizi kwa siku 14 ndipo hujulikana kama ana virusi, wanaopimwa wanapaswa kuwekwa karantini kwa siku hizo.

 “Tumeshangaa kupitia vyombo vya habari kumemsikia Mkuu wa Mkoa wa Arusha akieleza umma kuwa dereva aliyemwendesha Mtanzania wa kwanza aliyegundulika na virusi vya corona kuwa hana maambukizi yeyote, jambo la kujiuliza hapa je siku 14 zimetimia?,” amehoji.

Katika taarifa yake kwa umma, Paresso amesema, “Serikali ifanye jitihada za lazima na ziada Kuhakikisha kuwa kunakuwapo na maabara ya kupima sampuli za virusi katika hospitali zetu za mikoa na si utaratibu wa sasa wa kupeleka sampuli hizo kwenye maabara moja tu jijini Dar es Salaam.”

Amesema jambo hilo linaweza kuwa na upungufu mkubwa endapo wagonjwa wakiongezeka na kutumia maabara hiyo moja watashindwa kutoa majawabu kwa wakati kutokana na kuzidiwa na kiwango cha idadi kubwa ya wanaohitaji huduma hiyo pia kwa kuzingatia ukubwa wa nchi yetu sio sahihi kutegemea maabara moja tu iliyopo Dar es salaam.

“Serikali ituambie dawa za kutibu virusi hivi zipo? Na je zitatosheleza kwa kiwango gani? Na kama hazipo je, hatua gani zinachukuliwa kwa sasa kama sehemu muhimu ya kuweza kusaidia tatizo hilo,” amehoji Paresso

Msemaji huyo wa upinzani amesema, “kuhakikisha wataalamu wetu wa afya wanaotoa huduma katika maeneo yenye mlipuko wanalindwa kwa kupatiwa vifaa maalum vya kujikinga na maambukizi ya corona.”

Katika taarifa hiyo, Paresso anasema Serikali inapaswa kutoa msaada wa ziada katika vituo vya kulelea watoto yatima, vituo vya wazee na vituo vya vijana walioathirikana madawa ya kulevya kwa kuwapatia sanitizer na mahitaji mengine ya msingi kwa ajili ya kujilinda na virusi vya corona.

Amesema kwa kuzingatia kuwa janga hili linaendana na athari za kibiashara, uchumi na mahusiano mengine ya kidiplomasia.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka serikali ituambie ni kwa namna gani itakabiliana na athari za kiuchumi na kibiashara zitakazotokana na mlipuko wa ugonjwa huu ikiwamo ni hatua zipi za awali zinapaswa kuchukuliwa ili kunusuru uchumi wa nchi(National income) na wa mtu mmoja mmoja(household income),” amesema Paresso

Mwisho wa taarifa hiyo, Paresso anasema, “pamoja na hayo natoa wito kwa Watanzania wote kufuata ushauri wa kitaalamu unaotolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona. Na tunaitaka serikali kutoficha hali halisi ya mlipuko wa ugonjwa huu kwa maana ya idadi ya wagonjwa na vifo.”

Chanzo: mwananchi.co.tz