Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yatoa kauli kwa Upendo Peneza kutimkia CCM

Upenndo Pic Chadema yatoa kauli kwa Upendo Peneza kutimkia CCM

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Saa chache kupita baada ya wanachama watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, Upendo Peneza kutangaza kujiunga Chama cha Mapinduzi (CCM), Chadema kimewatakia kila la kheri.

Upendo na wenzake aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Mkoa wa Manyara, Benson Andrew na Onesfory Mbuya aliyewahi kuwa Katibu wa chama hicho Jimbo la Morogoro Kusini wamejiunga na CCM leo Jumatatu, Januari 22, 2024.

Wametangaza uamuzi huo mbele ya umati wa Wana-CCM katika shughuli ya mapokezi ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, makao makuu ya chama hicho, jijini Dodoma.

Upendo aliyekuwa Mweka Hazina wa Chadema Kanda ya Victoria na wenzake wamesema wamevutiwa na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kutokana na uamuzi huo, Mwananchi Digital limezunbumza na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliwaeleza mmoja baada ya mwingine huku akisema Upendo, “amehitimisha safari ya muda mrefu wa kuondoka.”

Mrema amesema ni kweli Upendo aliwahi kuwa mbunge, mgombea ubunge 2020 Geita Mjini na, “tulianza kujua ataondoka kwa sababu tulipokuwa tunafanya operesheni Kanda ya Viktoria, yeye kuna wanachama alikuwa anataka wawe viongozi kwa nguvu zote walishindwa.”

“Kwa hiyo leo amehitimisha safari. Tunawatakia kheri huko walikokwenda.”

Kuhusu Mbuya amesema, “sio mjumbe wa Baraza Kuu, chama Mkoa wa Morogoro kwa kuwa walimsimamisha tangu mwaka 2021 ukatibu wa Jimbo la Morogoro Kusini.”

Mrema amesema alisimamishwa, “kwa sababu baada ya sisi kuwafukuza wabunge 19, yeye aliendelea kufanya nao kazi. Baada ya kusimamishwa alibaki kuwa mwanachama.”

Wabunge hao 19 ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Halima Mdee.

Wengine ni Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnes Lambart, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa na Hawa Mwaifunga.

Wengine ni Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Mrema akimzungumzia Andrew alisema ni, “Ni kweli alichukua fomu kugombea ubunge 2020 na ni mwanachama wa kawaida na hana nafasi yoyote kwenye chama.”

Walichokisema Upendo, wenzake.

Wakizungumza kwa zamu kwenye mapokezi hayo ambayo Dk Nchimbi amewaambia wana-Dodoma hiyo ni zawadi kwao kwa mapokezi mazuri, Upendo amesema CCM ndiyo kwenye maendeleo.

"Sijaingia CCM kwa ajili ya mwanamke mwenzangu Rais Samia Suluhu Hassan, nimeingia CCM kutoka na maendeleo anayoyafanya ikiwemo kuleta maridhiano kwa vitendo,” amesema.

Amesema Rais Samia amekuwa alifanya kila jambo kwa vitendo, "wanamtukana lakini amekuwa hajibizani na zaidi ya yote anafanya kwa vitendo aliyoyaahidi," amesema Peneza.

Amesema wakati anaingia kwenye siasa zaidi ya miaka 15 iliyopita alimueleza baba yake mzazi ambaye alimshauri ajiunge na CCM.

"Sikukubaliana na wazo la baba nikamwambia najiunga Chadema naye alinipa baraka zake na fedha za kunisaidia. Leo nimeamua kujiunga CCM kwa ndio chama chenye mwelekeo wa maendeleo," amesema Peneza.

Amesema ajenda ya maandamano ya Chadema kuhusu miswada ya sheria ya uchaguzi iliyowasilishwa bungeni haina mashiko kwa sababu Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria bado inafanyia kazi maoni yaliyotolewa.

Peneza amesema hata yeye alishangaa namna watu wengi walivyojitokeza kutoa maoni kuhusu miswada hiyo na kwamba hiyo ni maana yake ndani ya nchi demokrasia imekomaa.

Kwa upande Andrew, amesema maendeleo yanayofanywa na Serikali ya CCM chini ya Rais Samia ndiyo yamemfanya ajiondoe Chadema na kujiunga na CCM.

Amesema ameingia Chadema akiwa mdogo mwenye umri wa miaka 12 na amekuwa mwanachama wa Chadema kwa zaidi ya miaka 14 hadi alipoamua kujiondoa jana na kujiunga na CCM.

Kiongozi mwingine wa Chadema, Onesfory Mbuya amesema amevutia na R nne za Rais Samia ambazo ni maridhiano, kuvumiliana, kujenga na mabadiliko.

Amesema suala la maridhiano ndio kimemvutia zaidi na kuamua kujiunga na CCM kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia.

Amesema aliingia Chadema mwaka 2004 na aliwahi kushika nafasi kadhaa za uongozi ikiwamo Katibu wa Chadema Wilaya ya Morogoro na pia kumsaidia wa kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live