Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yatangaza njia za kupita maandamano kwenda Umoja wa Mataifa

IMG 4548 John Mnyika.jpeg Chadema yatangaza njia za kupita maandamano kwenda Umoja wa Mataifa

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zikiwa zimebaki siku saba, kabla ya kufanyika kwa maandamano ya amani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kupinga miswada mitatu ya sheria za uchaguzi na ugumu wa maisha, chama hicho kimetaja maeneo yatakapopita na kumalizikia maandamano hayo ya Januari 24, 2024.

Januari 13, 2024 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza vuguvugu la kudai haki litakaloambatana na maandamano ya amani ili kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi kuhusu miswada mitatu.

Miswada hiyo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa, yote ya mwaka 2023.

Akizungumza na wanahabari leo Jumatano Januari 17, 2024, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema maandamano hayo ya amani yatakuwa na vituo viwili vikuu yakianzia maeneo ya Mbezi kribu na stendi ya mabasi na mengine yakianzia Buguruni, yote yatamalizikia ofisi za makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini Dar es Salaam.

Mnyika amesema maandamano hayo yatakayoanza saa tatu asubuhi yatakuwa na njia mbili ikiwemo ya Mbezi yakipitia Barabara ya Morogoro, Shekilango, Igesa- Sinza na kuishia Barabara ya Sam Nujoma ambako ujumbe wa maandamano utakapokelewa kwenye ofisi za UN.

“Tumeshapeleka barua kwa Jeshi la polisi kwa mujibu wa kifungu cha 11 (4) cha Sheria ya Vyama vya Siasa toleo la mwaka 2019 kuhusu kufanyika kwa maandamano haya, tumezitaarifu mamlaka mbalimbali za polisi kuhusu njia zitakazotumika katika maandamano ya amani.

“Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, taarifa za maandamano zinatolewa kwa wakuu wa polisi wa wilaya (OCD), tumeandika barua kwenda kwa OCD wa Gogoni, Buguruni, Oysterbay, Mburahati, Msimbazi, kisha nakala tumezipeleka kwa makamanda wa polisi wa mikoa ya kipolisi Ilala na Kinondoni,” amesema Mnyika.

Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mtatiro Kintikwi aliyesema, “kwa sasa nipo nje ya ofisi kidogo, ngoja nikirudi nicheki kama itakuwa imeshafika,” amesema Kamanda Kintiku.

Kwa mujibu wa Mnyika, ajenda kuu ya maandamano hayo ya amani ni kuitaka Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu haja ya kuondoa bungeni miswada ya sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa ili kuandikwa upya baada ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 1977.

“Pia tunaitaka Serikali itengeneza mpango wa dharura wa kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha kwa Watanzania na mfumuko wa bei nchini,” amesema Mnyika.

Hata hivyo, wakati Chadema ikiendelea na mipango hiyo, Serimali imemwishasema hakuna haja ya kuondoa miswada hiyo bungeni badala yake utoaji wa maoni unaendelea kwa mujibu wa tarabu.

Msemaji wa Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amelieleza wananchi hivi karibuni kuwa jambo la kufanya hivi sasa ni wananchi na wadau kutoa maoni na mapendekezo yatakayoboresha kilichopo katika miswada hiyo.

"Tutumie nafasi kutoa maoni yetu, kwa nini Serikali iondoe kitu walichokileta kukijadili kwa utaratibu wa kawaida na si hati ya dharura? Mkutano wa Ofisi ya Msajili ulikuwa mzuri na kulikuwa na sekretarieti ya kukusanya maoni, tutoe maoni ya kuboresha si kuiondoa bungeni au kufanya tukio lolote lisilorajiwa.

"Kwa nini uondolewe wakati kuna utaratibu mzuri umewekwa wa kutoa maoni, ingekuwa Serikali imeleta miswada kwa utaratibu usioruhusu maoni hapo watu wangezungumzia uwezekano wa kuondolewa miswada," amesema Matinyi.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametangaza kuwa Januari 23 na 24 siku ambayo yamepangwa maandamano, askari wa majeshi mbalimbali watakuwa wanafanya usafi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live