Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yataka wapigakura wenye sifa wajiandikishe

49437 CHADMA+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa wito kwa wananchi wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Uandikishaji wa majaribio unafanyika katika kata mbili kufuatia tangazo lililotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupitia kwa Mwenyekiti Jaji Semistocles Kaijage, ambapo unafanyika kwa siku nane kuanzia Machi 29 hadi Aprili 4.

Uandikishaji utaanza Ijumaa Machi 29, 2019 katika kata ya Kibutu iliyopo Kisarawe, mkoa wa Pwani na Kihonda Morogoro mjini.

Taarifa iliyotolewa Machi 28, 2019 na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Chadema, Tumaini Makene kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa uandikishaji huo ni muhimu. 

“Chadema inahamasisha wananchi kujitokeza na kujiandikisha kwa wingi, ikitambua pia kuwa NEC imekiuka Katiba ya nchi na Sheria ya Uchaguzi kupitia mamlaka ya kuratibu na kusimamia uandikishaji wa wapiga kura nchini,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imewataka waliofikisha umri wa miaka 18 au wanaotarajiwa kufikisha umri huo mwaka kesho wakati wa kupiga kura, wajitokeze katika maeneo hayo waandikishwe kupiga kura.

“Wote waliopoteza vitambulisho vyao na wale ambao vitambulisho vyao vimeharibika au wamehamia makazi katika maeneo hayo wafike katika vituo hivyo kwa ajili ya utaratibu wa kuandikishwa na kuhakiki taarifa zao,” amesema Makene.

Makene amesema katika taarifa hiyo kuwa tayari Chadema imeweka utaratibu wa kuwa na mawakala katika vituo vyote vya kuandikisha wapigakura kama taratibu zinavyoelekeza.

Amesema kwa kutambua umuhimu na unyeti wa uandikishaji wa wapigakura kama hatua muhimu katika mchakato wa uchaguzi, hasa Taifa linapojiandaa na uchaguzi mkuu, Chadema imejipanga kushiriki na kufuatilia shughuli hiyo kwa ukaribu na umakini unaohitajika.



Chanzo: mwananchi.co.tz