Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yataka mabadiliko mfumo wa stakabadhi ghalani

Chadema23 Tamko Chadema yataka mabadiliko mfumo wa stakabadhi ghalani

Wed, 3 May 2023 Chanzo: mwanachidigital

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya kimetoa siku 14 kwa Serikali kutengua kauli ya kuwataka wakulima kuuza zao la ufuta kwa mfumo wa stakabadhi ghalani katika Bonde la Songwe Wilaya ya Songwe mkoani humo.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwasote (China) ameliambia Mwananchi Digital leo Jumatano Mei 3, 2023 na kwamba wameanza kufanya mikutano ya hadhara katika Kata tano kueleza msimamo wao na kuungana na wakulima, wanununuzi na makampuni kupinga mfumo huo unaodaiwa ni kandamizi.

“Chadema tumeona ni vyema kuunga mkono wakulima kupinga kuuza ufuta kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwani umekuwa kandamizi kwao na kujikuta wakiwa na madeni mengi mara wanapoiuzia Serikali kwa kukopwa,” amesema.

Ameongeza kuwa “Hatutoweza kuvumilia kuona watu wanyonge wananyonywa kwani wanakuwa na changamoto kubwa katika uzalishaji na kutegemea kukopeshwa fedha kutoka kwa wanunuzi na makampuni cha kushangaza Serikali inaibuka wakati wa mavuno pasipo kujua hadha walizokumbana nazo,” amesema China.

Amesema Serikali kabla ya kuwataka wakulima kuingia katika mfumo huo ilipaswa kujua changamoto zao, kuwawezesha katika hatua za awali za kilimo na kuboresha miundombinu rafiki ya barabara na si kukurupuka kuangalia mapato wakati wapo walio wafikisha hapo wakulima.

“Sio tunapiga kampeni za kuwania Jimbo la Songwe, kama chama tuna simamia misingi ya Wananchi wa kipato cha chini na kutetea maslai yao hususan wanunuzi na makampuni ambao wamekuwa wakisaidia wakulima, kimsingi tunaimani ndani ya siku 14 Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan itatoa majibu ”amesema.

Mwasote amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa na malengo mazuri na wakulima lakini changamoto iko kwa watendaji wake wa chini hususan na baadhi ya watu kuingiza siasa kwa maslai yao binafsi na kwamba Chadema kinasema imetosha kwa wakulima na makampuni kunyanyasika.

Mwasote ametaja kata ambazo wameanza kufanya mikutano ya hadhara kuanzia leo Mei 3,2023 ni Kanga, Ifwenkenya, Igamba, Garula na Muheza ambako ndiko wananchi wake wanajihusisha na kilimo cha zao la ufuta sambamba na kuzungumza na wanunuzi.

Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa wanunuzi wa zao la Ufuta Mamlaka ya Mji wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya, Elisard Sinkwembe amesema kuwa Serikali inapaswa kuona namna gani mkulima ananyonywa kwa kuuza ufuta kwenye mfumo wa stakabadhi gharani.

Na kwamba asilimia kubwa ya wakulima hao wamekuwa wakitegemea wanunuzi kuwakopesha fedha wakati wa maandalizi ya kilimo misimu yote.

“Tunaunga mkono kauli ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuitaka Serikali kutengua mfumo wa mfumo wa Stakabadhi ghalani kwani siyo rafiki na unachangia kuzorotesha kilimo hicho na badala yake itengeneze mifumo rafiki na si unyonyaji na kuzorotesha wanunuzi na makampuni kutoka ndani na nje ya nchi ,” amesema.

Sinkwembe ameiomba Serikali inaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia suala hilo kwani kuna uwezekano mkubwa wakulima wakashindwa kuendelea kuzalisha ufuta kutokana na kushinikizwa kuuza kwa mfumo wa stakabadhi gharani,” amesema.

Awali Aprili 26, mwaka huu Mwananchi ikiripoti taarifa ya wakulima wa ufuta Mkoa wa Songwe kupinga msimamo wa Serikali kuwataka kuuza kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa madai ya kutokuwa rafiki ikiwepo utitili wa tozo ambao ni kandamizi kwao.

Chanzo: mwanachidigital