Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yasusia uchaguzi wabunge Eala

Chadema23 Tamko Chadema yasusia uchaguzi wabunge Eala

Mon, 5 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema chama hicho hakitashiriki uchaguzi wa kuwapata wabunge watakaoiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashiriki (Eala).

Uchaguzi huo utafanyika katika mkutano wa Bunge la Tanzania utakaoanza Septemba 13, 2022 jijini Dodoma.

Mnyika amesema vikao vya Chadema bado havijajadili msimamo wake kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambao walisema matokeo yake hawayatambui.

Katibu Mkuu huyo ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 5, 2022 wakati akizungumza na Mwananchi Digital, kuhusu ushiriki wa wao Eala baada ya vyama vya ACT - Wazalendo na CUF kukamilisha mchakato wa uteuzi wa majina ya wagombea wao watakaowakilisha vyama hivyo katika uchaguzi huo.

Wakati ACT-Wazalendo na CUF vikiteua wagombea wao leo Jumatatu CCM inamalizia mchakato wa uhakiki wa majina ya wagombea wao waliowasilisha vielelezo na sifa za kuwania ubunge wa Eala.

“Hatutashiriki, vikao vya chama havijabadili bado msimamo wetu kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Tunasisitiza kuharakishwa kwa mchakato wa kupata KatibaMpya,

“Pia kushughulikia wa athari na madhara yaliyotokana na uchaguzi mkuu wa 2020. Ni vema dhamira ya kufungua ukurasa mpya kuonyeshwa kwa haraka kwa masuala yenye kuhitaji utekelezaji wa Katiba na sheria mfano haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara,” amesema Mnyika.

Mbali na hilo, Septemba 14, mwaka 2021 Chadema kilisusia uchaguzi mdogo wa marudio wa jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga, kikisisitiza hakitashiriki mchakato wowote hadi Tume Huru ya uchaguzi itakapopatikana.

Pia Chadema kilisusia kikao cha ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa na wadau wa demokrasia uliofanyika jijini Dodoma na kufunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live