Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yakita mizizi ikijiimarisha kimataifa

CHADEMA MBELE Chadema yakita mizizi ikijiimarisha kimataifa

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezidi kujiimarisha katika siasa za kimataifa baada ya viongozi wake kufanya ziara ya nchini Marekani baada ya Ulaya.

Lengo la ziara hiyo ambayo sasa inafanywa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe inalenga kukutana na viongozi mbalimbali kujadiliana hali ya demokrasia, utawala wa sheria na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.

Mbowe aliondoka jana kwenda Marekani ikiwa imepita wiki moja imepita tangu makamu wake-Bara, Tundu Lissu aongoze ujumbe uliotembelea nchi mbalimbali barani Ulaya.

Mbowe ambaye ni Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Vyama vya Demokrasia Afrika (DUA) anakwenda kwenye ziara hiyo akiwa na kofia hizo mbili, DUA na Chadema.

Mfululizo wa ziara zinazofanywa na viongozi wa chama hicho barani Ulaya ni sehemu ya mkakati wa kuyaomba mataifa ya ng’ambo kuongea na Serikali kuangalia namna ya kulegeza vikwazo vinavyokwamisha shughuli za siasa nchini.

Miongoni mwa mambo hayo ni kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara, kufufuliwa kwa mchakato wa Katiba Mpya pamoja na kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utakaotanguliwa na wa Serikali za Mitaa mwaka mmoj akabla, yaani 2024.

Ni takriban miezi minane sasa tangu Chadema na Chama cha Mapinduzi (CCM) walipoanza kufanya vikao vya maridhiano kwa nia ya kuleta mwafaka wa kisiasa nchini lakini mazungumzo hayo hayajaleta tija iliyokusudiwa na wiki iliyopita, Lissu alilieleza gazeti hili kuwa mwezi huu wataamua kuendelea nayo au la.

Jana, kabla ya kuondoka nchini, Mbowe alisema “nakwenda kama mwakilishi wa bara zima la Afrika, sasa hivi nafanya siasa za Afrika…hatuishi kama kisiwa, tunaisha kama jamii ya kimataifa, kama unaishi na dunia kuna kusaidiana, kubadilishana mawazo.”

Kabla ya Mbowe hajazungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alitoa taarifa kwa umma kuhusu ziara hiyo akisema Mbowe atahudhuria kongamano la International Democrat Union (IDU) litakalodumu kwa siku tatu nchini Marekani ambako atakutana na kujadiliana na viongozi wenzake kuhusu hali ya siasa nchini.

“Kongamano hili litakalohudhuriwa na vyama wanachama wa IDU, viongozi wa Serikali, wabunge na maseneta wanaotokana na vyama wanachama wa IDU pamoja na taasisi za kimataifa, litahitimishwa na kikao cha Baraza la Uongozi la IDU Desemba 09,” alisema.

Mrema alisema Mbowe akiwa nchini humo anategemewa kuhudhuria kongamano lingine la mkutano wa Baraza la Uongozi la IDU kama mwenyekiti mwenza wa Democrat Union of Africa (DUA) na mmoja wa makamu wenyeviti wa IDU zaidi ya nafasi yake kama kiongozi wa Chadema.

“Mbowe atafanya mfululizo wa vikao na viongozi mbalimbali duniani pamoja na taasisi na mashirika ya kimataifa kuhusu hali ya kisiasa nchini. Kwa nafasi yake atakutana na mashirika na viongozi mbalimbali kujadiliana hali ya demokrasia, utawala wa sheria na maendeleo ya kiuchumi Afrika,” alisema Mrema.

Baada ya ziara hiyo, alisema Mbowe atazungumza na Watanzania waishio nchini humo kwenye mkutano utakaofanyika Desemba 10 jijini Washington DC.

Mbowe ameondoka wakati usiku wa kumkia jana, katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika, naibu wake-Zanzibar, Salum Mwalimu, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Pambalu na mjumbe wa kamati kuu, Zeudi Mvano waliokuwa pamoja na Lisssu wakirejea nyumbani.

Wakiwa na Lissu ambaye amebaki nchini Ubelgiji anakoishi, walitembelea mataifa mbalimbali ya Ulaya na Mrema alisema ujumbe huo uliokuwa Ulaya umerejea jana (juzi) usiku na mwenyekiti (Mbowe) anakwenda Amerika ambayo ni maeneo mawili yenye nguvu za kisiasa duniani.

“Umoja wa Ulaya na Marekani ni maeneo muhimu na tunatarajia mashinikizo tuliyokuwa tunayatoa huko nyuma kuhusu haki za siasa, madai ya Katiba Mpya, tumeshatoa muda wa kutosha kwa Serikali lakini hakuna mabadiliko yaliyofanyika,” alisema.

Wachambuzi watia neno

Mchambuzi wa sera za maendeleo nchini, Bubelwa Kaiza alisema mfululizo wa ziara hizo utasaidia kukitangaza Chadema kimataifa lakini si kuleta nafuu kwenye maisha ya Watanzania.

“Kufanya ziara ni jambo jema la kujiongezea marafiki nje ya nchi lakini inawezekana kusiwe na mabadiliko ya maana hapa nchini kwa sababu hoja hapa ni Katiba ambayo haiwezi kutatuliwa kwa kwenda Marekani au Ulaya isipokuwa itatatuliwa na wananchi wenyewe,” alisema Kaiza.

Alisema wananchi wanahitaji uelewa na msukumo utakaowafanya viongozi wanaotawala kuona kuna hatari iwapo hawatatekeleza matakwa yao.

“Sheria za vyama vya siasa nchini haziwezi kushughulikiwa na Bunge la Ulaya, wanatakiwa watengeneze presha ya ndani itakayosababisha sheria na kanuni nyingine zibadilishwe,” alisema mchambuzi huyo.

Ali Makame, mchambuzi wa siasa visiwani Zanzibar alisema ziara hizo ni hatua nzuri ya kutafuta mbinu za kuleta ufumbuzi wa yanayopigiwa kelele.

Viongozi wasimamishwa

Wakati hayo yakiendelea, kamati tendaji ya chama hicho knda ya Serengeti imewasimamisha viongozi wanne kwa kile kilichotajwa kuwa ni utovu wa nidhamu.

Viongozi hao pia wameondolewa kwenye makundi sogozi ya mtandao wa WhatsApp ya kamati tendaji na sekretatieti ya kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu wakitakiwa kusubiria uamuzi utakaotolewa na kikao cha kamati ya maadili kuhusu suala lao.

Waliosimamishwa ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi, katibu wa kamati ya wagombea wa kanda hiyo, Amos Chacha, Katibu wa Kamati ya Hamasa, Alfred Ngimba na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu, Joseph Martinus.

Taarifa zinasema viongozi hao wamesimamishwa kwa utovu wa nidhamu waliyoonyesha kwenye kikao cha kamati tendaji ya chama hicho kilichofanyika juzi.

“Kamati imeadhimia hivyo, Ntobi wa wenzake walikimbia kikao kabla hakijaisha bila kutoa taarifa kwa mwenyekiti (Gimbi Masaba) na hiyo taarifa ilikuwa ya ndani lakini nimeshangaa kuiona inasambaa mitandaoni,” alisema mjumbe mmoja.

Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Gimbi Masaba alisema kamati ilifanya uamuzi huo ili kutoa nafasi kwa kamati ya maadili na nidhamu kuwashughulikia viongozi waliokacha kikao hicho.

“Hata kama una dharura binafsi haimaanishi huwezi kumtaarifu mwenyekiti wa kikao, kitendo cha kutoroka kimyakimya bila taarifa na kufanya akidi ipungue huo ni utovu wa nidhamu na hatuwezi kujenga chama ambacho viongozi wake hawana nidhamu,” alisema Masaba.

Alipoulizwa iwapo viongozi hao walikiuka kanuni, Masaba alisema Chadema inajipanga kurejesha nafasi ilizopoteza katika uchaguzi uliyopita hivyo kamati haitosita kufuata miongozo ya vikao vya kikatiba ambavyo vinatakiwa kuwa na akidi iliyotimia.

“Kamati yetu ina wajumbe 30 siku hiyo nilikuwa na taarifa za wajumbe watano tu ambao walisema hawatokuwepo, wakati tunaanza akidi ilizidi nusu ya wajumbe lakini muda ulivyokuwa unazidi kwenda wajumbe walianza kutoroka ndiyo maana kikao kilisimama na kufanya uamuzi huo,” alisema Masaba.

Alisema Chadema kinafuata misingi ya haki na kama viongozi hao wanadhani wameonewa wasubirie kamati ya maadili kwani wao walitimiza wajibu wao tu wa kusimamia nidhamu kama inavyotakiwa.

Hata hivyo, Ntobi alisema “nimetumiwa tu ujumbe kwa simu kuwa nimesimamishwa bila kunieleza kanuni niliyovunja lakini kama nilivunja kanuni yoyote nipewe nakala ya maandishi ila ni kweli niliondoka mida ya saa 10 jioni baada ya tumbo kuvurugika.”

Kwa upande wake, Martinus alisema ameshtuka baada ya kuondolewa kwenye makundi sogozi ila anamtafuta katibu wa kanda hiyo, Mnyawami kujua sababu.

“Nilihudhuria kikao hadi saa 10 jioni kwa sababu nilikuwa na ratiba zangu nyingine nikaondoka baada ya kuona tumekamilisha kila kitu ila nashangaa nimetumiwa ujumbe na kuondolewa kwenye magrupu (makundi) ya WhatsApp,” alisema Martinus.

Chanzo: Mwananchi