MGOMBEA mwenza wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Salum Mwalim amesema endapo wananchi watakichagua chama chake na kushinda Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu na kuunda serikali, itatoa bima ya afya bure kwa kila Mtanzania.
Mwalim alisema hayo wakati akihutubia wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Shujaaa uliopo mjini Morogoro juzi.
Alisema lengo ni kumfanya kila wananchi apate fursa ya kugharamia matibabu hata yale ya gharama kubwa kama walivyo wananchi wa mataifa mengine wanavyofanya kwa wananchi wao.
“Ndiyo maana tunasema kila Mtanzania tutaweka utaratibu awe na bima ya afya ili aweza kuwa na uhakika wa afya yake,” alisema.
Pia, alisema endapo chama chake kitapata ridhaa ya kuchaguliwa na kuunda serikali itahakikisha hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizojengwa sehemu mbalimbali nchini zinapewa vifaa na vitendea kazi.
Mbali na vitendea kazi , pia itahakikisha zinakuwa na watumishi watakaotosheleza mahitaji ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Pia alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wenye sifa ya kupiga kura kujitokeza Oktoba 28, mwaka huu kuwachangua wagombea wa Chadema kuanzia urais , ubunge na udiwani.
Kwa upande wake, Mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kupitia chama hicho, Devotha Minja alisema endapo wananchi wa jimbo hilo wanamchagua awe mbunge wao , kipaumbele cha kwanza ni kuanzisha Saccos ya kutoa mikopo bila riba ili kuwawezesha kuendesha biashara zao na kukuza mitaji yao.