Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yajibu hoja za Lijualikali

MREMA NA SPIKA Chadema yajibu hoja za Lijualikali

Wed, 20 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeeleza kushangazwa kwake na kauli ya mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali kuwa chama hicho kinawakata wabunge sehemu ya mishahara yao kuchangia chama, kwa kuwa huo ni utaratibu wa wazi uliopo kwenye Katiba ya chama.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema kuhusu suala la hoja ya Lijualikali ni jambo la kikatiba na ni wajibu wa kila mwanachama kukichangia chama.

“Wapo ambao siyo wabunge na wanaendelea kuchangia chama pamoja na mapato yao madogo. Huyu anaijua vyema kabisa Katiba ya chama na amekuwa akichangia kwa utaratibu huo. Nadhani alikuwa anaigiza ili aweze kupata kazi aliyokuwa anaiomba huko aendako, ndiyo maana akatunga ule uongo bungeni,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu kama Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kama amerejesha fedha za Bunge kama alivyotakiwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema kuwa kwa sasa hawezi kulijibu suala hilo kwani wana mambo mengi ya kufanya kwa masilahi ya nchi.

“Hilo hatuwezi kuzungumzia suala hilo, kuna mambo mengi makubwa kwenye nchi ambayo tunashuguka nayo na si suala kama hilo,” alisema Mrema

Akizungumza bungeni juzi, Lijualikali (Chadema), aliangua kilio akidai kwamba kumekuwa na uonevu mkubwa ndani ya chama chake na ameomba nafasi ya kujiunga na CCM mara baada ya Bunge kuvunjwa Juni 19.

Pia mbunge huyo amedai kwamba wabunge wa Chadema wamechangishwa zaidi ya Sh bilioni nane kugharamia Mfuko wa Uchaguzi na walipohoji waliambiwa kwamba fedha hizo zimetumika kujenga chama.

Akizungumza jana kabla ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge, Lijualikali alisema Chadema mambo mengi hayaendi vizuri na mwenyekiti wa chama hicho amekuwa akikiendesha kidikteta.

“Watu wanaambiwa tumeingia kufuata posho, nimetukanwa sana, kama kuna watu wanawaza kuja hapa kwa ajili ya posho, mimi nimekuja hapa kwa ajili ya watu wa Kilombero. Nataka watu wajue hapakuwa na makubaliano na kulikuwa na amri na tulipohoji hakukuwa na majibu, hili ni agizo. “Mheshimiwa Spika, tulihoji tunaenda karantini siku 14 na baada ya siku 14 tunarejea wapi. Unapotuambia turudi kwa hoja gani.

“Mheshimiwa Spika, mimi nimeingia bungeni sijalala siku mbili maumivu, mimi nimekaa jela miezi sita, nimefungwa kwa sababu ya Chadema, leo nakuja kutimiza wajibu wangu naambiwa… (anaanza kulia).

“Mheshimiwa Spika, nimeumia ninapewa mashtaka kwenye redio, kwenye you-tube, hakuna barua ya kunishtaki, tunalilia katiba mpya, lakini katiba yetu tunaikanyaga.

“Tunalilia katiba ya nchi wakati ya kwetu tunaivunja, leo naonekana mtu wa ovyo kwa sababu nimekataa kitu ambacho naamini ni cha uongo,” alisema Lijualikali.

Alitolea mfano jinsi ambavyo mbunge wa CCM, Hussein Bashe alikuwa akiikosoa Serikali, lakini leo amekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, wakati hali ni tofauti kwa Chadema.

“Mungu ni mwema, hatuwezi kuwa chama cha demokrasia kama tunashindwa kufanya mambo madogo katika demokrasia, leo nakaa hapa nilikuwa namwangalia Bashe anavyoikosoa Serikali, lakini leo Bashe ni Naibu Waziri.

“Tukipima demokrasia ndogo tu, hivi kesho tukifanya demokrasia katika nchi yetu tutafanya mangapi, wabunge wanakuja inbox mtutetee, wanashindwa kumwambia mtu ambaye hana dola kwamba unakosea mzee, hana jeshi hana polisi hana nguvu yoyote, akipewa dola itakuwaje?” alisema Lijualikali.

Alihoji zilipo zaidi ya Sh bilioni nane ambazo wabunge walikuwa wakikatwa posho kuchangia Mfuko wa Uchaguzi Mkuu wa chama.

“Mheshimiwa Spika, wakati naingia bungeni wabunge wote walilkuwa wanakatwa laki tano kila mwezi kwamba kutakuwa na Mfuko wa Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kampeni na sisi ni vijana tumejitoa kutumikia chama chetu.

“Mimi nilifanya ubunge nikiwa na milioni sita peke yake ili tuweze kuchangiana, tunakuja kuuliza tunaambiwa hela hakuna zaidi ya bilioni nane.

“Unauliza mlisema tuweke hela kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, unajibiwa uchaguzi ni mchakato na tulinunua magari unauliza ruzuku imefanya kazi gani unaambiwa hii ni amri ya chama,” alisema Lijualikali.

Alisema katu hawezi kuendelea kuwepo katika chama hicho na atarudi Ifakara kufanya biashara.

“Mimi nipo tayari, nitarudi Ifakara nitalima mpunga nitafuga mbuzi, ng’ombe. Nitakuwa bodaboda, nitalima mchicha, mimi bado kijana, lakini siwezi kuendelea kutumika vibaya,” alisema Lijualikali.

Hata hivyo alisema kwamba kama CCM wapo tayari kumpokea yupo tayari kujiunga na chama hicho.

“Na Mheshimiwa Spika, niombe kama mtakuwa radhi kwa chama chako cha Mapinduzi (CCM), hata kazi yoyote nitafanya tu (wabunge wanashangilia). Nitaomba baada ya Bunge kuisha niwashukuru watu wa Kilombero,” alisema huku akianza kulia tena.

NDUNGAI ASISITIZA

Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Job Ndugai ameendelea kusisitiza kwamba Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema) arejeshe fedha anazodaiwa la sivyo hatua zaidi zitachukuliwa ili kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa.

Akizungumza na MTANZANIA jana kwa ajili ya kujua iwapo agizo lake alilolitoa juzi la kumtaka Mbowe arejeshe fedha hilo limetekelezwa au la, Spika Ndugai alisema hana taarifa rasmi za kilichoendelea kwa kuwa jana hakuwepo ofisini.

Alisema hata hivyo hana wasiwasi kwa kuwa maadamu fedha hizo ni za Serikali zitarudi tu na kuhusu namna gani zitarudi iwapo Mbowe hatazirudisha mwenyewe kwa hiyari yake, alisisitia kamba hakuna linaloshindikana katika hilo.

“Kutorudisha fedha hizi hadi akatwe ni aibu. Kwa mtu mzima na muungwana ni vyema kama unajua una fedha ambayo si halali yako uzirejeshe. Kwa Mbowe ni vyema tu atumie ustaarabu kurejesha hizo fedha, maana akisubiri kukatwa kama wanavyokatwa watu wanaofanya vibarua huko itakuwa ni fedheha kwake,” alisema.

Alisema kwa sasa hafikirii kuwa itafikia hatua ya kumkata kwenye mshahara au posho zake ila bado anaangalia nia nzuri zaidi ya kumfanya arejshe fedha hizo kwa taratibu zilizopo zinazohusiana na marejesho ya fedha za umma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live