Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yaituhumu CCM kupanga kuteka mawakala

10943 Chadema+pic TanzaniaWeb

Thu, 9 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeituhumu CCM kupanga njama za kuwateka mawakala wao katika kata ya Mawenzi Manispaa ya Moshi siku ya kupiga kura.

Hata hivyo, CCM kupitia kwa katibu wake wa Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabhia, wamekanusha tuhuma hizo, wakidai ni propaganda chafu ambazo hazikubaliki katika jamii ya wastaarabu.

“Hatujawahi kupanga wa wala hatutakaa tupange kuteka watu. Wapiga kura wataamua wenyewe na wao wajiandae kisaikolojia kushindwa na wasitafute sababu wala visingizio.

“Tangu mwanzo tulisema mikakati yao tunaijua. Mwanzo walipanga kuteka wagombea wao tulipowashtukia wakaahirisha na sasa wamekuja na mpango kuwa tunataka kuteka mawakala wao,” alidai Mabhia.

Akihutubia mkutano wa kampeni juzi jioni, meneja wa kampeni wa Chadema katika Kata ya Mawenzi, Frank Kagoma, alidai wamepata taarifa za kutekwa kwa mawakala wao na kuonya juu ya jambo hilo.

Akimnadi mgombea wao, Afrikana Mlay, Kagoma alidai endapo itatokea mawakala wao hata mmoja tu atatekwa ili asiweze kusimamia zoezi hilo la kura, Serikali inayoongozwa na CCM isiwalaumu.

Madai hayo yalitiliwa nguvu na katibu wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema aliyedai Chadema imejulishwa juu ya njama hizo pamoja na mipango ya vurugu na kwamba wamejiandaa kuikabili.

Akizungumza katika mkutano huo, mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Grace Kiwelu, alisema wao wameweka mawakala makini na waadilifu ambao hawawezi kufika bei na kusisitiza ushindi ni wao.

Alidai pia wanazo taarifa kuwa baadhi ya viongozi wa CCM na makada wao wanawatisha wafanyabiashara kuwa wasipichagua CCM watafungiwa biashara zao.

Alipoulizwa juu ya tuhuma hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah aliwataka Chadema kutoa taarifa polisi kama wana taarifa za kweli badala ya kutoa tuhuma majukwaani.

Chanzo: mwananchi.co.tz