Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yaitaka NEC kusimamia haki uchaguzi mdogo

Thu, 12 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia haki katika uchaguzi mdogo wa Ubunge na udiwani.

Uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 12, 2018, ni wa jimbo la Buyungu, Kigoma na kata 77.

Aliyekuwa mbunge wa Buyungu, (Chadema) Kasuku Bilago, alifariki dunia Mei mwaka huu.

 Uchaguzi wa madiwani unafanyika baada ya wengi, kuhama vyama vya upinzani na kuhamia CCM wakidai wanaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 12, 2018 jijini Dar es Salaam amesema kutokuwa na uchaguzi huru kunaweza kusababisha machafuko katika nchi.

Dk Mashinji amesema katika uchaguzi huo wa marudio kumeanza kujitokeza vitendo vya ukiukwaji  wa taratibu za uchaguzi ikiwamo kughushi saini za viongozi ili kuhalalisha wagombea katika Halmashauri ya Tunduma mkoani Songwe.

Amesema wagombea wa Halmashauri hiyo wamepitishwa kwa barua ya kughushi na kuviomba vyombo vya dola kuwachukulia hatua wote waliohusika.

"Tunahitaji kuwa na Tume huru ya uchaguzi na katika uchaguzi huu Tume isimamie haki na hizi figisufigisu zilizoanza kujitokeza izisahihishe," amesema Dk Mashinji

Dk Mashinji amebainisha kasoro zingine ni wagombea wao kukamatwa na kunyang'anywa fomu.

''Uchaguzi huru hudumisha amani na kama hakuna uchaguzi huru unaweza kusababisha uvunjifu wa amani."amesema

Chanzo: mwananchi.co.tz