Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yainyooshea kidole NEC, CCM Arusha yateua waliojiuzulu Chadema

11344 Chadema+pic TanzaniaWeb

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chadema imeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha inafanyia kazi upungufu ulioanza kujitokeza katika uchaguzi wa ubunge na madiwani unaotarajia kufanyika Agosti 12.

Hivi karibuni, NEC ilitangaza uchaguzi mdogo kufanyika katika kata 77 na Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma ambako aliyekuwa mbunge, Kasuku Bilago (Chadema) alifariki dunia Mei 26.

Julai 11, NEC ilitangaza mabadiliko katika maeneo ya uchaguzi na kuongeza kata mpya mbili huku ikiahirisha uteuzi katika kata nne. Mabadiliko hayo yalifanya kata za udiwani kuwa 77 badala ya 79 za awali.

Jana, katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji alisema wamenusa hujuma mbalimbali ikiwamo kughushiwa kwa nyaraka za majina ya wagombea wao.

Dk Mashinji alisema hujuma hiyo imefanyika katika Mji wa Tunduma mkoani Songwe baada ya nyaraka za wagombea waliopitishwa na mkutano ngazi ya wilaya kughushiwa.

“Ili kuondoa mtafaruku huo, kama kuna mtanziko, mimi mwenyewe Dk Vicent Mashinji, katibu mkuu wa Chadema niliandika barua ya kutawambulisha wagombea kwenye kata hizo tano,” alisema.

Aliwataja waliopitishwa na kata zao katika mabano kuwa ni Osiah Kibwana (Kaloleni), Boniphace Mwakabanje (Majengo), Eliah Lonje (Sogea), Ally Sinkologo (Mpemba) na Hitler Haonga (Mwaka Kati).

“Kwa kuwa hili ni suala la kughushi, tumeripoti kituo cha polisi na kupewa namba MMB/PE/32/2018, kama mkurugenzi (mtendaji wa Halmashauri ya Tunduma) anasema anaitambua hiyo barua ailete na awaeleze polisi amepata wapi mamlaka na hilo suala tunawaachia polisi kuchunguza hilo, lakini ukiiangalia hiyo barua haina mfumo wa barua zetu za Chadema,” alisema Dk Mashinji.

“Tumeanza kuona huu uchaguzi utakwenda kuvurugwa na tumeandika barua kwa mkurugenzi wa Tume (ya Taifa ya Uchaguzi), tukimweleza mapungufu ambayo yanafanywa na wasimamizi wake wa uchaguzi.”

Katibu mkuu huyo alidai kuwa hujuma wanazofanyiwa Tunduma, zinaendelea katika baadhi ya kata nchini na kuiomba NEC kuhakikisha inasimamia uchaguzi huo kwa kufuata sheria zilizopo ili kuepuka uvunjifu wa amani.

Mwananchi lilizungumza na mkurugenzi wa NEC, Athuman Kihamia aliyesema malalamiko hayo hayana maana kwa sasa kwa kuwa hata uteuzi wa wagombea haujafanyika hadi Julai 14.

Kihamia aliwashauri Chadema kusubiri uteuzi ufanyike huku akisisitiza kuwa hata wakipeleka malalamiko yao kwa sasa hayatakuwa na maana.

Waliojiuzulu Chadema

Katika hatua nyingine, CCM mkoani Arusha imetangaza majina ya wagombea wa udiwani katika kata 20 kwa ajili ya uchaguzi huo.

Waliopitishwa ni madiwani 19 waliojiuzulu Chadema kisha kujiunga na CCM.

Katibu mwenezi wa CCM mkoani humo, Shaaban Mdoe alisema jana kuwa, wagombea hao wamepitisha na wajumbe wa Halmashauri ya CCM mkoa katika kikao kilichofanyika jana.

Chadema bado

Kwa upande wa Chadema, hadi jana walikuwa bado katika vikao vya kupitisha wagombea wao.

Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Aman Golugwa alisema wamejipanga kutetea kata zao na wanatarajia kupitisha wagombea makini.

“Tunajipanga kufanya vizuri tunajua uchaguzi utakuwa mgumu kwani tuna uzoefu na uchaguzi uliopita wa marudio,” alisema Golugwa.

Nyongeza na Mussa Juma, Arusha.

Chanzo: mwananchi.co.tz