Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yadai kubaini vituo hewa 15 vya kupigia kura Ukonga

16649 Pic+chadema TanzaniaWeb

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku chache kufanyika uchaguzi mdogo Jimbo la Ukonga, uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umedai umebaini vituo hewa 15 vya kupigia kura jimbo humo.

Akizungumza jijini Dar es Salaamm  leo, Katibu Kanda ya Pwani wa chama hicho, Casmir Mabina alisema wamefanya uchunguzi na kubaini vituo hivyo hewa ambavyo kwenye daftari la wapiga kura la mwaka 2015 havikuwepo.

‘’Tumebaini ongezeko la idadi ya vituo vya kupigia kura katika jimbo la uchaguzi Ukonga kutoka vituo 659 vilivyotumika katika uchaguzi mkuu wa 2015 hadi kufikia vituo 674 katika uchaguzi huu mdogo unaotarajiwa kufanyika Septemba 16.”

‘’Ongezeko la vituo hivi  limeleta maswali mengi kwetu na kwa wadau wa siasa, hivyo tunaitaka ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Ukonga itoe ufafanuzi,’’alisema Mabina.

Alisema walishaandika barua kwa msimamizi wa ofisi ya Uchaguzi jimbo hilo lakini hakuna majibu yoyote waliyopewa mpaka sasa kuhusu sheria na taratibu iliyotumika kuongeza idadi ya wapiga kura.

Alisema kutokana na ukimya huo chama kimeamua kuwaapisha mawakala wake wote ambao watasimamia uchaguzi huo hata hivyo hewa.

“Tumejipanga kudhibiti kura hewa na kutaka kuwabaini hao wapiga kura ambao watakuwa hewa kama je ni wananchi wa Ukonga au wanatoka sehemu nyingine?” alisema.

Aidha, Mabina alisema hakuna majina yaliyobandikwa kwenye maeneo ya vituo hivyo, jambo ambalo alidai linaleta ukakasi kwani sheria inasema majina yabandikwe kabla ya siku saba za kufanyika uchaguzi.

Kwa upande wake Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Jimbo la Ukonga, Hilary Baina alisema hakuna orodha ya vituo iliyoongezwa kama inavyodaiwa bali orodha iliyotumika ni ileile ya mwaka 2015.

“Tumeshawaita (Chadema) tukaongea nao na tukakubalina sasa hili la orodha wanayosema ni ipi tena wakati tumeshawajibu na hata kuhusu majina tumeshasema tutabandika wakati ukifika,’’ alisema  Baina.

Chanzo: mwananchi.co.tz