Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema yaahidi kutatua changamoto Buyungu

9899 Pic+buyungu TanzaniaWeb

Fri, 3 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewahakikishia wakazi wa kata ya Gwanumpu na Kanyonza zilizopo jimbo la Buyungu mkoani Kigoma kwamba changamoto ya huduma mbovu za jamii inayowakabili itatatuliwa haraka ikiwa watamchagua mgombea wa chama hicho.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni kwenye vijiji vya Rusenga, Bukirilo na Kanyonza, viongozi wa Chadema wameahidi kushirikiana na jamii kuondoa kero ya maji, madarasa na nyumba za walimu.

Mgombea ubunge wa Chadema jimbo la Buyungu, Eliya Michael alisema akichaguliwa atahakikisha wakazi wa kata hizo wanapata maji ya uhakika na hivyo kuondokana na adha ya muda mrefu inayowakabili.

Alisema wananchi wote hawana budi kupata huduma za kijamii kwa vile wanalipa kodi ili serikali ilete maendeleo, lakini baadhi ya vijiji bado havijapata miradi ya maji na hata zahanati.

Aliwataka wananchi kuendelea kufyatua matofali kwa ajili ya kuimarisha ‘benki zao za matofali’, jambo linalorahisisha ujenzi wa miradi kama ya nyumba za walimu, vyumba vya madarasa, zahanati na ofisi za umma.

Katika mikutano yake mbalimbali, amewahakikishia kwamba atatumia ruzuku ya mfuko wa jimbo kusaidia miradi ya kimkakati ndani ya jimbo pamoja na kusaidia vikundi vya ujasiriamali vya wanawake na vijana.

Mkurugenzi wa Itifaki na Bunge wa Chadema, John Mrema amesema wabunge wa Chadema wamejiandaa kumpatia ushirikiano wa kutosha mgombea huyo ili aweze kutekeleza vema majukumu yake ya kibunge na kijamii kwa ajili ya maendeleo ya Buyungu.

Amesema licha ya kuwekewa mizengwe na vigingi bado wataendelea kuibana serikali ndani na nje ya Bunge hadi hapo wananchi watakapopata huduma bora za kijamii.

Katibu wa Chadema mkoa wa Kigoma, Shaban Madede amewaomba wakazi hao kumuenzi mbunge wa zamani, marehemu Kasuku Bilago kwa kumchagua Eliya Michael.

Chanzo: mwananchi.co.tz