Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema wazungumzia majibu ya NEC kwa Marekani

12326 CHADEMA+PIC.png TanzaniaWeb

Fri, 17 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chadema kimesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) inapaswa kulaumiwa kwa kuvuruga uchaguzi mdogo uliofanyika Agosti 12, 2018,  kuorodhesha  baadhi ya matukio iliyodai yalilenga kuwakandamiza wagombea wa chama hicho na wanachama.

 

Leo Alhamisi Agosti 16, 2018 chama hicho kimetoa taarifa kwa vyombo vya habari na kubainisha kuwa baadhi ya maeneo wagombea wake walienguliwa katika mazingira ya kutatanisha, hata walipojaribu kuhoji hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

 

Katika uchaguzi huo kwenye jimbo la Buyungu na kata 36, CCM kiliibuka na ushindi huku vyama vya upinzani vikishindwa kuibuka na ushindi katika kata zote na jimbo hilo.

 

Chama hicho kimesema  taarifa iliyotolewa na NEC kujibu tamko la Ubalozi wa Marekani  kuhusu uchaguzi huo mdogo,  haiakisi  ukweli wa mambo na badala yake ilipotosha kuhusu kilichotokea kwenye mchakato wa uchaguzi huo.

 

Taarifa hiyo iliyotolewa na ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene inasema NEC imeshindwa kusimamia uchaguzi uwe huru na haki, kutokana na ama kutokuwa na uwezo au kufumbia kwa makusudi hila na njama zilizokuwa zikifanyika kuharibu na kuvuruga uchaguzi huo.

 

“Jamii ya watanzania, jumuiya ya kimataifa na dunia nzima iliona na kushuhudia kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari ikiwemo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii jinsi ambavyo NEC ilishindwa kusimamia uchaguzi uwe huru na haki,” imesema.

 

“Mathalani  wagombea udiwani wa Chadema katika kata tano Tunduma walinyimwa fomu zao za kugombea kwa makusudi kabisa kisha fomu hizo wakapewa watu wengine (wanaodaiwa hawajulikani).”

 

Imesema, “kwa kutumia mbinu za kijinai zinazohusisha kughushi. Kama hiyo haitoshi wagombea wetu wakaanza kusakwa na kukamatwa na polisi na kubambikiwa tuhuma za jinai.”

 

Mbali na hoja hizo, Chadema imesema imeshangazwa na namna NEC ilivyohoji Marekani ilitumia utaratibu gani kupata taarifa ilizotoa kuwa uchaguzi uligubikwa na vitendo vya vurugu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.

 

“Swali hilo la NEC linaibua swali jingine,  je mamlaka zilizoharibu na kuvuruga uchaguzi huo zilifanya hivyo kwa sababu zilijua hakuna waangalizi wa kimataifa? Je zilifanya hivyo kwa sababu zilijua habari za matukio hayo hazitaufikia ulimwengu ambao hautakaa kimya,” imesema taarifa hiyo.

 

Hata hivyo, jana Agosti 15, 2018 NEC iliutaka ubalozi huo kuthibitisha inachokieleza juu ya uchaguzi huo, ikisema uchaguzi mdogo huwa hauna waangalizi wa kimataifa na kuhoji ubalozi huo umetoa wapi taarifa hizo na hayo iliyoyaona ni kwa kutumia utaratibu upi na sheria ipi.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz