Hatimaye Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetinga katika ofisi za Umoja wa Mataifa (UN), jijini Dar es Salaam, baada ya kuandamana Kwa takriban saa tano.
Msafara wa Chadema ulioongozwa na viongozi wake waandamizi uliwasili UN majira ya saa 15.10 mchana, tangu ulipoanza saa 10.00 asubuhi katika maeneo ya Buguruni na Mbezi jijini humo.
Baada ya Chadema kuwasili ofisini hapo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alimpa utaratibu wa kuingia ndani humo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, mbele ya afisa wa UN aliyekuja kuwapokea.
Kamanda Muliro alimweleza Lissu kuwa, kwa mujibu wa itifaki na taratibu za UN, inatakiwa viongozi wanne wa chama hicho akiwemo mwanamke mmoja, waingie ndani kuwasilisha malalamiko yao kisha wakimaliza watatoka nje kuzungumza juu ua kile kilichojiri.
“Mheshimiwa tulikuwa na jambo moja linalofahamika la itifaki, kwa mfumo uliopo wanasisitiza kwamba watu wanne ndio wanaoingia mule akiwemo katibu Mkuu, mwenyekiti Makamu na mwanamke mmoja. Watu wengine watabaki nje watasubiri mambo mengine,” amesema Kamanda Muliro.
Lissu alikubali masharti hayo na kuahidi kwamba Chadema itatekeleza. “Hatuwezi kuvunja itifaki za UN sisi ni chama cha siasa tunaotekeleza sheria hakuna shaka tutafuata,” amesema Lissu alimweleza afisa wa UN baada ya kupewa maelekezo hayo.
Kwa sasa msafara wa maandamano ya Chadema uko nje ya ofisi hizo wakisubiri kinachoendelea.