Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema wasema bado Sh90 milioni kuwatoa jela viongozi wote

98770 Mbowe Ruma+pic Chadema wasema bado Sh90 milioni kuwatoa jela viongozi wote

Fri, 13 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kinahitaji Sh90 milioni ili kukamilisha fedha za kuwalipia faini viongozi wake watano waliopo gereza la Segerea.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Machi 12, 2020 na mwenyekiti wa kamati ndogo ya rasilimali fedha ya Chadema, Ezekia Wenje kuhusu utaratibu wa kuwachangia viongozi wa chama hicho.

Viongozi wanane wa Chadema pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji Jumanne Machi 10, 2020 walihukumiwa kulipa faini ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.

Washtakiwa hao wakiongozwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walilazimika kwenda jela baada ya kushindwa kukamilisha taratibu za kulipa faini hiyo waliyohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Baada ya hukumu hiyo iliyosomwa  na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Chadema walianza kuchangishana fedha kwa ajili ya kuwalipia faini viongozi wake hao.

Leo wabunge watatu: Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda) na Esther Matiko wametoka jela baada ya kulipa faini ya Sh110 milioni.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement

Dk Mashinji alitoka jana baada ya kulipa faini ya Sh30 milioni,  fedha zilizochangwa na wanachama wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole.

Wenje amesema hadi jana jioni walikuwa wamechangiwa Sh234 milioni, “Sh110 milioni  zimetumika kuwatoa Mdee, Bulaya, Matiko.  Kwa sasa tumepata namba ya kuwalipia faini  wengine. Tutalipa Sh100milioni na ikiwezekana leo jioni au kesho watatoka.”

“Tunaamini Watanzania wameendelea kuchanga. Bado tuna upungufu wa Sh90milioni, tunaamini hadi Ijumaa tutakuwa tumemaliza kuwatoa wote.”

 

Chanzo: mwananchi.co.tz