Dar es Salaam. Wakati takribani wanachama 16 wa Chadema wakikamatwa na polisi huku baadhi yao wakidaiwa kujeruhiwa, chama hicho kimewaomba polisi kuwapeleka Hospitali waliopata majeraha.
Chama hicho kimesema wanachama wake, wakiwemo viongozi wamejeruhiwa katika gereza la Segerea walikokwenda kumchukua mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyetoka jela baada ya kulipa faini ya Sh70 milioni.
Kati ya wanaoshikiliwa ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; Meya wa Ubungo, Boniface Jacob; katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo; diwani wa Tabata, Patrick Asenga na mjumbe wa baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Hadija Mwago.
Akizungumza leo jioni Ijumaa Machi 13, 2020 naibu katibu mkuu wa Chadema (Bara), Benson Kigaila amesema waliojeruhiwa hadi sasa hawajapelekwa hospitalini, baadhi ya wanachama majina yao hayajawekwa wazi.
“Licha ya kuwajeruhi na kuwakamata wengine ambao idadi yao haijajulikana kikamilifu, magari mengine ya chama yaliyokuwa yameegeshwa mbali na gereza hilo katika stendi ya Mbuyuni nayo yalitolewa upepo na askari kuyalinda,” amesema
Amesema askari hao walitumia nguvu bila sababu ya msingi, “tukitoka hapa mimi na wanasheria wa chama tutakwenda kujua baadhi ya watu wamepelekwa wapi.”
Habari zinazohusiana na hii
- Mbowe atoka jela
- Mbowe alipa faini, muda wowote kutoka jela
- Wanachama wa Chadema watawanywa kwa mabomu ya machozi gereza la Segerea
- Halima Mdee, Bulaya na Meya Ubungo wakamatwa