Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema wamzulia jambo Mgeja

Chadema wamzulia jambo Mgeja

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shinyanga. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Shinyanga kimemkana aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja kuwa hakuwa mwanachama wa chama hicho ila alikuwa kama mshenga wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Ijumaa Machi 8, 2019 Katibu wa Chadema mkoa wa Shinyanga, Zakaria Obadi amesema Mgeja hakuwa mwanachama wa Chadema ila alikuwa mshenga tu wa Lowassa hivyo walishangaa kuona anatangaza kwa waandishi wa habari anahama Chadema na kuhamia CCM.

Obadi amesema Mgeja ametangaza akisema alihamia mwaka 2015 lakini chama kinajua alikuja kama mshenga kwa sababu hakukabidhiwa hata kadi ya Chadema hivyo chama kilikuwa hakimtambui kama ni mwanachama.

"Sisi tulishangaa tu kumuona na yeye anatangaza kukihama chama chetu kwani tunajua alikuwa kiongozi wa CCM Mkoa, alipohama Lowassa na yeye akamfuata kama mshenga ndio maana hakuwa na kadi yoyote, Lowassa yeye yuko sawa kwa kusema amerudi nyumbani kwanza yeye alikuwa na kadi ya Chadema," amesema Obadi.

Amesema wao kama viongozi wa mkoa wana haki ya kumjibu Mgeja kwani hastahili kujibiwa makao makuu, kwa sababu hakuwepo hata kwenye taarifa za chama hata kuvaa mavazi ya Chadema hajawahi, wao wanawatambua wanachama.

"Tunaomba wasiwe wanatumia chama chetu kama ngazi ya kuwanusuru mambo yao, kwa kweli hatujawahi kumkabidhi kadi yetu, alikuwa anazungumzia ruzuku ambayo ilipatikana kwa vyama vya Ukawa, lakini ruzuku ina sheria yake sisi tunajua lakini yeye alikuwa akizungumza tu alikuwa hajui chochote lakini tunamsamehe," amesema Obadi.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Shinyanga, Hamis Omary amesema wahamiaji wanafanya siasa za ajabu ajabu hivyo wao wako imara na wana imani kubwa kwamba watafanya vizuri kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

Mgeja alitangaza kuhamia Chadema mwaka 2015 mara baada ya Lowassa kufanya hivyo Julai 28, 2015 lakini hivi karibuni, Lowassa alitangaza kurudi CCM na sasa Mgeja naye amechukua uamuzi kama wa Lowassa.

Katika uchaguzi mkuu 2015, Lowassa aligombea urais kupitia Chadema na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi ambapo Mgeja alikuwa miongoni mwa watu waliozunguka na Lowassa kumnadi karibu nchi nzima.



Chanzo: mwananchi.co.tz