Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema wamjaribu bosi mpya NEC

11121 Chadema+pic TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitashiriki uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani ikiwa ni sehemu ya kumpima mkurugenzi mpya wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Athuman Kihamia.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimesema pia kitautumia uchaguzi huo wa Jimbo la Buyungu na kata 79 utakaofanyika Agosti 12, kufanya siasa za majukwaani ambazo tangu utawala wa Awamu ya Tano uingie madarakani zimezuiwa.

Uchaguzi wa Buyungu unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wake, Kasuku Bilago wa Chadema kufariki dunia Mei 26 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Uchaguzi wa madiwani utafanyika katika halmashauri 43 zilizopo katika mikoa 24 ya Tanzania Bara kutokana na baadhi ya madiwani kuhama vyama na wengine kufariki dunia.

Uchaguzi huo ni wa kwanza kwa Kihamia ambaye Julai Mosi aliteuliwa na Rais John Magufuli kuchukua nafasi ya Ramadhani Kailima aliyehamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kuwa naibu katibu mkuu.

Chadema imewahi kumlalamikia Kailima ikidai kutowatendea haki katika chaguzi kadhaa zilizopita kiasi cha kususia baadhi ya chaguzi.

Katika uchaguzi wa madiwani kwenye kata 43 wa Novemba mwaka jana, Chadema iliilalamikia NEC kwa kutowatendea haki hali iliyowafanya kujitoa katika uchaguzi wa udiwani kata tano za Arumeru jijini Arusha.

Wakati Chadema wakijitoa, Kihamia alikuwa mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Arusha.

Kutokana na kilichotokea Novemba mwaka jana, Chadema ilisusia uchaguzi mdogo wa majimbo ya Longido, Songea Mjini na Singida Magharibi na kata kadhaa ikidai Tume isingewatendea haki.

Hata hivyo, katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni na Siha, Chadema ilishiriki na kuibua malalamiko ya kutotendewa haki, ikiwamo kucheleweshewa barua za mawakala wa usimamizi wa uchaguzi.

Uamuzi wa Chadema kushiriki uchaguzi wa Agosti 12 ulifikiwa katika kikao cha siku mbili cha Kamati Kuu kilichohitimishwa juzi chini ya mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema chama hicho kitashiriki uchaguzi huo ikiwa ni kipimo cha mkurugenzi mpya wa NEC.

“Tutashiriki uchaguzi huo na tutautumia uchaguzi huo kumpima huyu mkurugenzi mpya dhidi ya Kailima mtangulizi wake,” alisema Mrema.

Mrema alisema Kamati Kuu ya Chadema imempitisha Elia Kanjero kuwa mgombea ubunge jimbo la Buyungu na utaratibu wa kupata wagombea katika kata 79 unaendelea.

Pia alisema baada ya kuwa wamezuiwa kufanya mikutano ya hadhara, watautumia uchaguzi wa kata 79 kufanya siasa na kuwaeleza wananchi kile ambacho kinafanywa na Serikali.

“Uchaguzi wa madiwani tutashiriki na kama unavyojua, hizi kata 79 ziko katika mikoa 24 kwa hiyo ni kama uchaguzi wa nchi nzima. Kama wametuzuia mikutano ya siasa, tutashiriki ili kuwaeleza wananchi kile kinachofanywa na Serikali,” alisema Mrema.

Alisema katika uchaguzi huo watakuwa tayari kushirikiana na chama chochote ambacho kitakuwa tayari vikiwamo vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unaoundwa na CUF, NLD, Chadema na NCCR-Mageuzi.

Kuna uwezekano wa Kanjero kuchuana na Christopher Chiza wa CCM ambaye mwishoni mwa wiki aliongoza kura ya maoni akifuatiwa na Aloyce Kamamba na Emmanuel Gwegenyeza.

Fomu ya matokeo ambayo gazeti hili imefanikiwa kuiona, Chiza aliyewahi kuwa mbunge jimboni humo amepata kura 145, Kamamba kura 46 na Gwegenyeza kura 41.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kakonko, Abdul Kumbuga alisema kura hiyo ya maoni ni mapendekezo, hivyo wanasubiri uteuzi utakaofanywa na vikao vya ngazi ya juu ya chama hicho tawala.

Chanzo: mwananchi.co.tz