Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema walianzisha tena bungeni, CCM waja juu

15701 Pic+chadema TanzaniaWeb

Thu, 6 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mvutano mkali kati ya wabunge wa upinzani na wale wa CCM, jana ulitikisa kikao cha kwanza cha Bunge wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa mwaka 2018, hasa kuhusu uhalali wa Rais John Magufuli kutangaza manispaa kuwa jiji.

Kwa nyakati tofauti, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na Spika wa Bunge, Job Ndugai walilazimika kuingilia kati kuweka mambo sawa hoja zilizokuwa zikitolewa na wapinzani waliodai kuwa suala la Serikali kuhamia Dodoma halipo hata katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano na wa mwaka mmoja.

Aprili 26, katika hotuba yake ya dakika 31 aliyoitoa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kuadhimisha Sherehe za Muungano, Rais Magufuli aliutangaza mji wa Dodoma kuwa jiji la sita likitanguliwa na Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Mbeya na Arusha.

Kutokana na hatua hiyo, mipango mbalimbali imewekwa na halmashauri ya jiji katika kuhakikisha Serikali na wafanyakazi wanaohama kutoka jijini Dar es Salaam wanapata huduma zinazohitajika na kwa wakati.

Hoja za wabunge

Katika mjadala huo mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema uamuzi wa Rais kutangaza Dodoma kuwa jiji haukufuata sheria.

Akizungumzia Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 2008 ambayo inazungumzia vigezo vya manispaa kutangazwa jiji, pamoja na kuipa mamlaka Bunge kutangaza alihoji ni lini Bunge lilipelekewa muswada wa sheria ambao uliinyanyua Dodoma kuwa jiji.

Kabla ya Mdee kuchangia mjadala huo, akisoma maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni mbunge wa viti maalumu (Chadema), Sophia Mwakagenda alieleza jinsi wapinzani wanavyopitia kipindi kigumu, akidai baadhi wananunuliwa lengo likiwa ni kuuhadaa umma kufurahia utendaji kazi wa Serikali.

Wakati akiendelea kuzungumza alikatishwa na Mhagama aliyemtaka kujikita katika hoja iliyopo mezani kwa kutojadili mambo yasiyokuwapo.

Mhagama pia alimtaka kufuta kauli kuwa viongozi wa Serikali wanawanunua wabunge wa upinzani.

Pia, waziri huyo aliomba utaratibu wa Spika kuhusu mtu anayelidanganya Bunge na kujadili suala ambalo halijaletwa mezani kama la mjadala na kuzungumzia jambo ambalo liliamuliwa katika mikutano ya Bunge iliyopita.

“Nirudi katika kanuni ya 64 (b), hoja hii inayozungumzwa hapa ni tamko la Dodoma kuwa Makao Makuu na si tamko la kuwa jiji. Kwa hiyo hii pia ni uvunjifu wa kanuni, lakini kanuni ndogo ya 64 (c) jambo hili la Dodoma kuwa jiji lilishatolewa maelezo katika mkutano uliopita, kwa hiyo kulirudisha leo ni ukiukwaji wa kanuni,” alisema Mhagama.

Wakati akieleza hayo, mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko alimtaka Mhagama kuacha kuichambua hotuba yao kwani ilikuwa bado haijasomwa.

Baada ya Mhagama kumaliza, Ndugai alimtaka Mwakagenda kuendelea kwa kuzingatia yaliyoelezwa na waziri huyo.

“Natumaini umesikia yote uliyoambiwa, unasemaje kuhusu hayo uliyoambiwa, karibu,” alisema Ndugai.

Katika majibu yake, Mwakagenda alisema hotuba hiyo ni ya upinzani siyo ya CCM, kauli ambayo ilimuibua tena Ndugai, “Hii hotuba ni ya msemaji mkuu na kwa maana hiyo msemaji mkuu ni wewe, si ya kambi. Sasa mambo yaliyozungumzwa hapa ni ya msingi, hatuwezi kuyadharau. Inatakiwa kwa kweli tujielekeze kwa kilichoko mezani.”

Ndugai alisisitiza, “Kilichoko mezani si uchaguzi, sijui nani kanunuliwa sijui kamnunua nani. Je, tukisema twende maadili (Kamati ya Maadili), ukathibitishe nani alitoa shilingi ngapi. Jielekeze kwenye hoja iliyopo mezani.”

Baada ya maelezo hayo ya Spika, Mwakagenda alisema alichokuwa akizungumza ulikuwa utangulizi wake kama wengine walivyokuwa wakianza kwa kumpongeza Christopher Chiza aliyechaguliwa hivi karibuni kuwa mbunge wa Buyungu.

Wabunge CCM

Mbunge wa Chilonwa, Joel Mwakanyaga alisema kwa kiasi kikubwa kutungwa kwa sheria hiyo kutalifanya jiji hilo kutochezewa kwa kuwa ni makao makuu ya nchi.

“Tunaifanya hii sheria iwe na ugumu kwa mtu kuja kusema kama makuu ya nchi yawe sehemu nyingine, maana tukiliacha hili akaja mwingine akasema tuhamishe wabunge wakakubali gharama zitakazotumika zitaathiri Watanzania,” alisema.

Mbunge wa viti maalumu, Fatma Toufiq alisema mchakato huo ni mzuri na Serikali inapaswa kuweka mkakati wa wilaya za Dodoma kupanda miti zaidi ya 1,500 ili jiji listawi vizuri.

Mbunge wa viti maalumu, Felister Bura alisema Hayati Mwalimu Nyerere hakukosea kuweka mkakati wa Dodoma kuwa makao makuu.

Waibua tukio la Lissu

Katika kipindi cha jioni cha Bunge, wabunge John Heche (Tarime Vijijini-Chadema) na Hamidu Bobali (Mchinga-CUF), walitumia tukio la kupigwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kupinga hoja iliyotolewa na baadhi ya wabunge kuwa miongoni mwa vigezo vya Dodoma kuifanya kuwa makao makuu ya nchi ni usalama, wakisisitiza kuwa tangu tukio hilo hadi sasa hakuna aliyekamatwa.

Aitaja Zanzibar

Mbunge wa Malindi (CUF), Ali Salehe alisema muswada huo haukuishirikisha Zanzibar.

Alisema mtindo wa kutoishirikisha Zanzibar katika sheria zinazohusu Muungano si mzuri na ndiyo maana imekuwa ikikataliwa na Baraza la Wawakilishi.

“Mfano sheria ya deep sea (bahari kuu) ilipitishwa kimabavu hapa ikaenda kule Baraza la Wawakilishi ikakataliwa,” alisema.

Hata hivyo, baada ya kumaliza kuzungumza Spika Ndugai alimjibu mbunge huyo kuwa wabunge waliopo bungeni ni wawakilishi wa wananchi na pande zote mbili zinawakilishwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz