Dodoma. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimejitoa kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 na kuwataka wagombea wake walioenguliwa kutokata rufaa.
Uamuzi huo umetangazwa leo Alhamisi Novemba 7, 2019 na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe baada ya kumalizika kwa kikao cha dharura cha kamati kuu mjini Dodoma. Kabla ya kutangaza uamuzi huo wajumbe wa kikao hicho walikutana na wabunge wa chama hicho.
Mbowe amesema hadi jana Jumatano asilimia 60 ya wagombea wake ndio waliofanikiwa kuchukua na kurejesha fomu za uchaguzi huo.
“Katika mazingira hayo walilazimika kukaa viongozi wa chama baada ya vikao imeonekana ni busara kwa chama chetu kutobariki uchaguzi wa kihuni. Na kuendelea kushiriki katika uchaguzi huu ni kuhalalisha ubatili,” amesema Mbowe.
Amesema watatoa maelezo kwa viongozi na wagombea kusitisha ushiriki katika uchaguzi huo.
“Waachane na kukata rufaa, kuweka pingamizi. Hatupo tayari kubariki ubatili huu. Hatutajitoa katika ujenzi wa kidemokrasia kwa kujitoa katika uchaguzi huu,” amesema Mbowe.