Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema, wadau watoa maoni kauli ya Nec, taarifa ya Marekani

12335 Pic+chadema TanzaniaWeb

Fri, 17 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chadema, wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wanaharakati wametoa maoni juu ya taarifa ya ubalozi wa Marekani na ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuhusu uchaguzi mdogo wa Agosti 12 wakiwa na mitazamo tofauti.

Juzi, ubalozi wa Marekani ulitoa taarifa ukieleza kuwa uchaguzi huo mdogo wa ubunge wa Jimbo la Buyungu na udiwani katika kata 36, uligubikwa na vurugu na ukiukwaji wa sheria.

Hata hivyo, Nec ilitoa ufafanuzi kuhusu madai hayo na kuutaka ubalozi huo uthibitishe ulichokieleza kwa kuwa uchaguzi mdogo hauna waangalizi.

Baada ya ufafanuzi huo wa Nec, jana Chadema ilitoa taarifa ikisema Tume hiyo inapaswa kulaumiwa kwa kuuvuruga uchaguzi uliofanyika huku ikiorodhesha baadhi matukio iliyodai yalilenga kuwakandamiza wagombea wake na wanachama.

Katika taarifa yake, chama hicho kilisema kuna baadhi ya maeneo wagombea wake walienguliwa katika mazingira ya kutatanisha na hata walipojaribu kuhoji hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Kimedai Nec ilishindwa kusimamia uchaguzi uwe huru na haki, kutokana na ama kutokuwa na uwezo au kufumbia macho kwa makusudi hila na njama zilizokuwa zikifanyika kuuharibu na kuuvuruga.

“Jamii ya Watanzania, jumuiya ya kimataifa na dunia nzima iliona na kushuhudia kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari ikiwemo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii jinsi ambavyo Nec ilishindwa kusimamia uchaguzi uwe huru na haki,” inadai taarifa hiyo.

“Mathalan wagombea udiwani wa Chadema katika kata tano Tunduma walinyimwa fomu za kugombea kwa makusudi, kisha fomu hizo wakapewa watu wengine kwa kutumia mbinu za kijinai zinazohusisha kughushi.”

“Kama hiyo haitoshi wagombea wetu wakaanza kusakwa na kukamatwa na polisi na kubambikiwa tuhuma za jinai.”

Mbali na hoja hizo, Chadema ilisema katika taarifa yake kuwa, imeshangazwa na namna Nec ilivyohoji Marekani kwamba ilitumia utaratibu gani kupata taarifa ilizotoa kuwa uchaguzi uligubikwa na vitendo vya vurugu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.

“Swali hilo la Nec linaibua swali jingine, je mamlaka zilizoharibu na kuvuruga uchaguzi huo zilifanya hivyo kwa sababu zilijua hakuna waangalizi wa kimataifa?” ilihoji taarifa hiyo.

“Je zilifanya hivyo kwa sababu zilijua habari za matukio hayo hazitaufikia ulimwengu ambao hautakaa kimya?”

Wachambuzi wazungumza

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini na wasomi walitoa mtazamo wao kuhusu taarifa zote mbili.

Mhadhiri mwandamizi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Abdul Sherrif alisema huenda yaliyoelezwa na Marekani yakawa na ukweli ndani yake kwa vile sehemu kubwa ya kile kilichoendelea kwenye uchaguzi huo kilikuwa wazi katika vyombo vya habari.

Alisema Marekani na mataifa ya Ulaya yamekuwa yakipendelea kuona uwepo wa demokrasia ya kweli na pindi yanapoona kumejitokeza hali ya upande mojawapo kuminywa ni wepesi kutoa matamko ya kukemea.

“Kama sisi Tanzania hatutaki kuona matamko yao, basi tukatae kupokea misaada yao, vinginevyo tukubaliane na misingi ya kidemokrasia na kufuata maelekezo yaliyopo kwenye Katiba na sheria inayoruhusu watu kuwa na mikutano ya hadhara na kukusanyika,” alisema Profesa Sherrif.

Alisema ingawa Nec ilihoji Marekani ilitumia utaratibu gani kupata taarifa za kuwepo kwa vurugu kwenye uchaguzi huo, lakini katika dunia ya sasa huenda Taifa hilo lilikuwa na watu wake waliokuwa wakifuatilia na pia uwezekano wa kutumia vyombo vya habari.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Dk Parit Saruni alisema suala la uchaguzi ni la kidemokrasia, hivyo unapaswa kuendeshwa kwa kufuata sheria na kanuni.

Alisema vyama vinapaswa kuwa huru na kupambana kwa haki katika uwanja wa kisiasa bila upande wowote kupendelewa.

Hata hivyo, alidai wapinzani wakati mwingine huingia kwenye uchaguzi huku wakiwa tayari wamejijengea picha ya woga wa kuibiwa na hii inatokana na matukio ya siku za nyuma.

“Siasa za sasa zimebadilika sana.... wakati mwingine wapinzani wanapoingia kwenye uchaguzi tayari wana fobia (kuibiwa)na hali hii inawafanya wajihami kwani mara nyingi huko nyuma wamedai kuibiwa,” alisema mhadhiri huyo.

Alisema vyama vya upinzani vinaundwa na watu wazima wenye akili na hivyo wanapolalamika huenda kukawa na ukweli ndani yake.

Chanzo: mwananchi.co.tz