Mwanza. Wakati Waziri wa Tamisemi, Seleman Jaffo akiagiza wagombea walioenguliwa kupewa haki ya kusikilizwa rufaa zao, wagombea wa vyama vya upinzani walioenguliwa wilayani Tarime hawajapewa taarifa za kuenguliwa kwao ili wakate rufaa.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumatano Novemba 6, 2019 katibu wa Chadema mkoa wa Mara, Heche Chacha amesema kwa kukosa taarifa hizo, wagombea zaidi ya 800 wa chama hicho walioenguliwa wameandika barua za kukata rufaa bila kujua sababu za kuenguliwa kwao.
“Kwa mujibu wa kanuni wagombea wote, wawe ameteuliwa au kuenguliwa wana haki ya kuona orodha ya majina ya uteuzi. Kwa Tarime hilo halijafanyika. Kibaya zaidi wasimamizi wasaidizi wamefunga ofisi zao kutwa nzima ya Novemba 5, 2019 ambayo ndio ilikuwa siku ya kupokea rufaa,” amesema Heche.
Ametaja kata zilizoathirika zaidi kwa wagombea wa Chadema wote kuenguliwa bila kupewa sababu ni Manga, Muriba na Kemambo.
“Sisi ni wadau wa amani ya Taifa na katika suala hili la uchaguzi tunachotaka ni haki kwa vyama na wagombea wote kwa mujibu wa katiba, sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi. Raha ya kushinda ni kushindana kwa haki,” amesema Heche.
Akizungumzia madai hayo, msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Peter Nyanja amesema ofisi yake inaendelea kusikiliza majibu ya pingamizi zote na kuahidi haki itatendeka kwa vyama na wagombea wote kwa mujibu wa sheria. “Mchakato wa uteuzi umekamilika jana Novemba 5, 2019, leo tunashughulikia pingamizi katika ngazi ya wasimamizi wasaidizi na uamuzi utatolewa na pande zote zitakuwa na haki ya rufaa,” amesema Nyanja
Akizungumzia wagombea kukosea kujaza fomu na taarifa muhimu kwa mujibu wa sheria na kanuni msimamizi huyo amesema, “changamoto ninayoiona ni vyama kutowaelimisha wagombea wao, binafsi nilikaa na viongozi wa vyama vyote vya siasa na kuelimishana kanuni, kifungu kwa kifungu na kurasa kwa kurasa. Inashangaza kuona makosa kwenye fomu.”
Ametaja baadhi ya makosa yaliyofanywa na wagombea kuwa ni pamoja na kutaja majina ya vitongoji visivyokuwepo kwenye eneo lake la, kutoeleza kazi halali ya kipato huku baadhi wakiomba kugombea ujumbe bila kueleza ni kundi lipi kati ya ujumbe wa jumla au viti maalum.
Kuhusu orodha ya wagombea, Nyanja amesema ilibandikwa katika mbao za matangazo kwa mujibu wa kanuni ya 18 (1) hadi (4), sura ya 287 ya kanuni ya uchaguzi.
“Orodha hiyo (ya wagombea walioteuliwa na kuenguliwa) ikieleza sababu iwapo mgombea ameenguliwa inatakiwa kubandikwa kati ya saa 2:00 asubuhi na saa 10:00 jioni. Kama ilibanduliwa labda ni kutokana na jazba au hamaki za walioenguliwa na wafuasi wao,” amesema.
Msimamizi wa Halmashauri ya Tarime mji, Jane Tungu hakuwa tayari kuzungumzia madai ya wagombea kutoka vyama vya upinzani kutotendewa haki ikiwemo orodha ya uteuzi kutobandikwa kwenye mbao za matangazo.