Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema wadai kuporwa ushindi

17915 Pic+chadema TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi amesema kilichofanyika kwenye uchaguzi mdogo katika kata tatu jijini humo na maeneo mengine juzi kuwa, “ni uporaji wa matokeo ya wapinzani.”

Mbunge huyo maarufu kwa jina la Sugu alitoa kauli hiyo jana jijinihapa katika mkutano wa waandishi wa habari huku akiapa kwamba mwisho wa CCM umekaribia kwa kuwa wananchi si wajinga.

Sugu akiwa na mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa walikuwa wanazungumzia mchakato wa uchaguzi katika kata za Maanga, Iwambi na Nsalaga jijini Mbeya na ya Nkuyu wilayani Kyela ambazo zimechukuliwa na CCM.

Pamoja na kata hizo, CCM pia ilishinda majimbo mawili ya Monduli na Ukonga pamoja na kata 20 zikiwamo za wilayani Hai mkoani Kilimanjaro ambako ni jimbo la mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Hata hivyo, katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alieleza kufurahia ushindi wao akisema ni matokeo ya kazi nzuri ya Rais John Magufuli kushughulikia shida za watu.

“Rais wetu ambaye ni mwenyekiti wa chama amefanya kazi kubwa na kudhihirika kwa matokeo chanya, ndiyo maana leo tunashuhudia CCM ikishinda kwa kishindo,” alisema Polepole alipoulizwa ni kwa vipi chama hicho kinashinda kila uchaguzi unaoitishwa tangu 2015.

Kuhusu vyama vya upinzani, Polepole alisema vimeshindwa kutofautisha mambo mazuri na badala yake wameendelea kulaumu kila kukicha hata pale CCM inapofanya vizuri.

“Wanashindwa kutofautisha ni wakati gani wanakosoa au ni wakati upi wanaunga mkono, hakuna mchawi, wanapaswa kujitafakari upya la sivyo wataendelea kulalamika,” alisema.

Hata hivyo, mbunge wa Mbeya Mjini, Sugu alisema wanaamini waliporwa ushindi kwani matokeo yaliyotangazwa na yaliyobandikwa vituoni hayaendani na uhalisia wa kura zilizopigwa.

Mchungaji Msigwa

Akizungumza katika mkutano huo, Msigwa ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini alisema kilichofanyika katika uchaguzi huo hawakubaliani nacho na sasa wanapaswa kuchukua hatua dhidi ya ule aliouita kuwa ni uonevu.

Alisema katika uchaguzi huo, ilionekana wananchi kukosa morali ya kupiga kura, hivyo wasimamizi walifanya uchakachuaji kwa kuongeza idadi ya wapiga kura wakati wa kujaza fomu za matokeo ili ionekane watu wengi walijitokeza.

Msigwa alisema, “Kama chama ni vyema tukatafakari upya na kuchukua hatua stahiki dhidi ya dhuluma hizi, vinginevyo tutakuwa tunapoteza muda na tunapeleka watu wetu wanateseka bila sababu.”

“Hivyo sisi Chadema Kanda ya Nyasa tunakaa kikao na tutatoka na maazimio ya kukishauri chama chetu ni hatua gani tunapaswa kuzichukua badala ya kuendelea kulalamika.”

Demokrasia

Msigwa alisema suala la kupigania demokrasia na utawala bora nchini siyo la Chadema au viongozi wa chama hicho pekee, bali ni la watu wote.

Aliwataka Watanzania kuamka na kuwa kitu kimoja kwa mustakabali wa demokrasia ya kweli na kupinga matumizi mabaya ya vyombo vya dola na madaraka.

Akizungumzia hatima ya upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Msigwa alisema harakati wanazozipigania ni pana zaidi kuliko kufikiria nafasi za ubunge wa mtu.

Alisema wanachokipigania ni kutaka utawala bora, demokrasia na haki za binadamu na hawaendeshi harakati kwa kutaka kulinda nyadhifa walizonazo.

“Wengine tumeanza kupambana na hali hii hata kabla ya kuwa wabunge, Sugu ameanza kuimba muziki akiwa na miaka 21 akipigania harakati za nchi hii,” alisema.

“Kwa hiyo msidhani mapambano haya ni kwa sababu ya kulinda nafasi za ubunge, tunataka haki za watoto wetu, watoto wenu na wa vizazi vijavyo.”

Wafuasi wa Chadema

Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Mjini, Obadia Mwaipalu alisema siku moja kabla ya uchaguzi na siku ya juzi ya uchaguzi wenyewe, wafuasi wengi wa chama hicho walikamatwa na hadi jana walikuwa hawajatolewa mahabusu.

Wakati huohuo, CCM nao walilalamika wafuasi wao kupigwa na kuumizwa wakidai waliofanya hivyo ni wafuasi wa Chadema, hivyo walilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linawachukulia hatua.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, William Nkhambaku alisema, “kupata ushindi huo haikuwa kazi rahisi, lakini niseme tuna vijana wetu walipigwa na kuumizwa vibaya hapa Mbeya mjini na kule Kyela ambako hali ilikuwa mbaya sana. Hivyo tunalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linawachukulia hatua waliohusika.”

Polisi wazungumza

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alisema vyama vyote - CCM na Chadema vinalalamikiana kufanyiana fujo bila kuwa na uhalisia wa suala lenyewe.

Akizungumzia kukamatwa kwa wafuasi wa vyama hivyo, alisema watu waliokamatwa na polisi hawakuwa na nembo za chama wala hawakujitambulisha.

“Hawa viongozi ni vyema wakaja ili wakatuonyeshe watu wao ni kina nani, maana kule (Mbeya Mjini) tulikamata watu wengi kwa makosa mbalimbali, hivyo wanaosema ni wafuasi wao waje ili wakatuonyeshe pale kituoni,” alisema.

Matei alisema watu walio na uhakika nao ni wanne kuwa ni wafuasi wa Chadema ambao walikamatwa Kyela wakati wakielekea eneo la kutangazia matokeo wakiwa na bastola, cheni, mizinga ya nyuki na ‘mizula’ ya kininja.

Msimamizi wa Uchaguzi Jiji la Mbeya, James Kasusura alisema leo atakutana na waandishi wa habari ili kuzungumzia mchakato mzima wa uchaguzi ulivyokwenda.

Chanzo: mwananchi.co.tz