Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema kuvaa nguo nyeupe wakisubiri hukumu ya viongozi wao

98284 Pic+chadema Chadema kuvaa nguo nyeupe wakisubiri hukumu ya viongozi wao

Mon, 9 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani  kimewataka wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania  kuanzia leo Jumamosi Machi 7, 2020 kuvaa nguo nyeupe au kufunga kitambaa cheupe kama ishara ya kutaka haki itendeke katika hukumu ya viongozi wa chama hicho Machi 10, 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katibu wa kanda hiyo,  Hemed Ali ametoa wito kwa wanachama wote kufanya hivyo kwa kuwa haki ni ya kila mtu.

Viongozi wanane wa Chadema pamoja na katibu mkuu wa zamani wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria na kusababisha woga na hofu kwa wakazi wa Kinondoni na kifo cha Akwelina Akwilini.

Jana viongozi wakuu na wabunge wa Chadema walifunga kazi baada ya kuwasilisha hoja zao za majumuisho katika kesi ya jinai inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wameiachia mahakama kufanya kazi yake.

Viongozi hao ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Wengine ni naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) na mbunge wa Tarime Mjini; Halima Mdee (mbunge wa Kawe); Ester Bulaya (Bunda); John Heche (Tarime Vijijini).

Pia Soma

Advertisement
"Mavazi hayo meupe yatakuwa yakiashiria kupinga uonevu, watu tujitokeze kwa wingi siku ya hukumu pale mahakamani. Watakaoshindwa kukusanyika katika ofisi za Chadema basi wafanye midahalo ya haki siku hiyo.”

"Kuna wanawake zaidi ya 5,000 wanatoka mikoani wanakuja Dar es Salaam kwa ajili ya siku ya wanawake kesho, tumeongea na Baraza la wanawake Chadema wanawake hao wabaki hadi Machi 10 ili tuungane nao mahakamani," amesema Hemed.

Amesema siku hiyo ni siku ya kuonyesha amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania ili kupigania amani ya nchi aliyodai kuwa inapatikana ikiwa kuna haki.

"Hatupendi amani ya nchi hii iharibike lakini vilevile hatupo tayari kuona viongozi wa chama chetu wanaonewa, kesi yao hii ni kesi ya kisiasa," amesema.

Amedai  kuwa hukumu yoyote ya kuwatia hatiani viongozi hao itazima amani ya nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz