Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema kuunda ‘NEC’ ya mfano, kufungua tena kesi

42099 PIC+CHADEMA Chadema kuunda ‘NEC’ ya mfano, kufungua tena kesi

Mon, 18 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema imefikia maazimio mawili; kufungua kesi ya kupinga mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa mara itaposainiwa, na kuandaa rasimu ya muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi kwa lengo la kuibua mjadala.

Mabadiliko hayo, ambayo yamekuwa yakipingwa na vyama vya upinzani tangu hatua za awali ikiwa ni pamoja na kufungua kesi, yalipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano lililopita na sasa yanasubiri hatua ya Rais kuisaini kabla ya kutangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali.

Pia, muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) umekuwa ukipingwa, hasa na vyama vya upinzani kutokana na viongozi wake kuteuliwa na Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama cha siasa ambacho pia kinashindana, huku wasimamizi wa uchaguzi kuwa ni wakurugenzi wa wilaya ambao pia ni wateule.

Lakini kamati hiyo ya Chadema imesema itachukua hatua kukabiliana na sheria hiyo pia kutoa picha ya jinsi NEC inavyotakiwa iundwe.

“Mahakama ina mamlaka ya kuondoa vipengele vyote ambavyo vinaminya haki za binadamu, lakini pia vinavyokiuka Katiba ya nchi,” katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji aliwaambia waandishi wa habari jana baada ya Kamati Kuu ya Chadema kuazimia mwishoni mwa wiki.

“Hata tulipoenda kusajili kesi ya kupinga muswada tuliambiwa tusubiri iwe sheria.”

Muswada huo ulipitishwa siku chache baada ya Mahakama Kuu kutupa shauri la kikatiba la kupinga Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018, liliofunguliwa na viongozi watatu wa vyama vya upinzani.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Dk Benhajj Masoud baada ya kukubaliana na hoja mbili za pingamizi la Serikali kati ya 10 za kupinga shauri hilo kusikilizwa.

Naye makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema sheria hiyo itanyonga demokrasia.

“Tulishirikiana na wadau kupinga muswada huo, lakini hatukufanikiwa. Sasa tutafungua kesi ya kupinga sheria yenyewe itakapoanza kutumika kwa kuwa sasa Katiba itakuwa inakiukwa,” alisema Profesa Safari, ambaye amebobea katika sheria.

Shauri hilo la kikatiba lilifunguliwa Mahakama Kuu na wanasiasa watatu, wakioongoza na kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, kwa niaba ya muungano wa vyama 10 vya upinzani.

Walikuwa wakipinga kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kinachozuia muswada kupingwa mahakamani, wakiiomba mahakama itamke kuwa kinakiuka Katiba.

Pia, walikuwa wakipinga muswada huo wakidai unakiuka haki za kikatiba za kisiasa kwa kuwa unazifanya shughuli za kisiasa kuwa jinai na unampa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama.

Katika azimio jingine, Profesa Safari alisema kuna changamoto katika muundo wa NEC na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2002, hivyo mabadiliko yanatakiwa kufanyika ili kuwa na utaratibu utakaokuwa huru na haki.

Alisema chama itaandaa rasimu ya muundo wa tume kwa kushirikiana na wadau wengine, kama vyama vya siasa kwa lengo la kuibua mjadala wa kitaifa.

Profesa Safari alisema mabadiliko ya muundo huo yatahimiza kutangazwa kwa mshindi wa kweli katika uchaguzi kwa kuwa masuala ya kulinda kura hayapo popote hata Uingereza na Marekani ambako amewahi kuishi.

“Hakuna mtu anayelinda kura. Hata rafiki yangu Edward Lowassa nilimwambia siku moja kulikuwa na uchaguzi unafanyika Monduli akasema atapeleka morani, nikamwambia rafiki yangu wewe utaibiwa kisayansi tu hakuna cha morani wala nini,” alisema.

Mikutano ya hadhara

Pia, Dk Mashinji alisema chama hicho kinafanya uratibu na kupanga ratiba kwa ajili ya kuanza mikutano ya hadhara kama walivyoazimia Zanzibar.

“Tulikuwa na shughuli za kuimarisha chama na mambo mengine ya ndani, ndiyo maana hatukufanya mikutano, lakini sasa tunafanya maandalizi. Mikutano ni haki ya kikatiba hata aliyeizuia alifanya utashi wake binafsi,” alisema Dk Mashinji.

Alisema vyama vilijikuta vikitii amri isiyo halali kisheria na Serikali ilitumia hoja kuwa wapinzani wanatumia mikutano hiyo kutukana viongozi, wakati hawafanyi hivyo kwa kuwa chama kina sera ambazo kinataka kuzieleza kwa wananchi.Alisema viongozi wa CCM sasa wanafanya mikutano ambayo Serikali yao iliizuia, lakini imejikita katika kejeli na kukashifu watu.



Chanzo: mwananchi.co.tz