Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema kupambana na ‘madiwani wake’ 23 uchaguzi wa Agosti 12

11402 Pic+chadema TanzaniaWeb

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Ndani ya miaka miwili, Chadema imepoteza madiwani 50 kutokana na sababu mbalimbali huku wengi wakijiunga na CCM na kupitishwa kuwania tena udiwani kwa tiketi ya chama hicho tawala, na kuibuka na ushindi.

Ukiacha chaguzi ndogo zilizopita ambazo baadhi ya madiwani hao walipitishwa na CCM kugombea, katika uchaguzi utakaofanyika Agosti 12, tayari chama tawala kimewapitisha wagombea 23 ambao awali walikuwa madiwani wa Chadema.

Kufuatia hali hiyo, wachambuzi wa masuala ya siasa waliozungumza na Mwananchi wamekosoa hamahama hiyo ya madiwani, kushauri kutolewa kwa elimu ya uraia ili kila mwananchi atambue thamani ya kura yake na wagombea kujua wajibu wao kwa wananchi.

Wamesema elimu hiyo itaondoa wimbi la madiwani kuhama vyama vyao bila sababu za msingi.

Wakati jijini Arusha CCM ikitangaza wagombea katika kata 20, huku 19 kati yao wakiwa ni waliokuwa madiwani wa Chadema, mkoani Manyara chama hicho tawala kimewapitisha wagombea watano; wanne wakiwa ni waliokuwa Chadema na mmoja alikuwa diwani wa ACT-Wazalendo.

Wachambuzi watoa ya moyoni

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema Tanzania bado haijawa na demokrasia ya kufanya siasa kwa kuongozwa na misingi ya kiitikadi.

“Katika hali ya ushindani, kila chama kinatumia mbinu kinazodhani zitakiwezesha kupata ushindi. Ni ushindani kweli, lakini hauna mashiko, viongozi waongozwe na itikadi zao na siyo upepo unavyokwenda,” alisema Dk Bana.

Hata hivyo, mwanazuoni huyo alisema ni haki ya kiongozi anayejiuzulu kwenda chama kingine anachotaka na kugombea na kwamba siku zote demokrasia ni gharama, hivyo Taifa likitaka kuwa na demokrasia likubali gharama.

“Demokrasia inapendwa sana lakini ni ghali. Nadhani ili kuondokana na wimbi la madiwani kuhama na kisha kugombea tena kwa chama kingine, elimu ya uraia iendelee kutolewa wapigakura na wagombea watambue wajibu wao,” alisema.

Akiwa na mtazamo kama huo, mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema wananchi ndiyo wenye uamuzi wa mwisho wa kuwawajibisha wanasiasa wa aina hiyo kwa kutowapigia kura

Alisema licha ya kuisaliti jamii, wanasiasa hao wanadhihirisha kuwa hawana dhamira ya kuwawakilisha, bali kuwakilisha vyama ambavyo wanaviamini zaidi.

Alisisitiza kwamba vyama ni njia ya kufikia malengo ya uwakilishi.

“Huwa ninajiuliza sana, hawa watu wanachaguliwa vipi kwa mara ya pili? Jambo hilo linaibua mjadala juu ya demokrasia yetu. Tuwe wazalendo, tuijenge nchi yetu, siasa zisiturudishe nyuma,” alisema Salim.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema kwenye siasa kuna mbinu za kimkakati zinazotumika, lakini kwa kinachofanyika sasa siyo kitu kizuri na hakifai kwenye nchi ya kidemokrasia. Alisema walipokutana na viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alimuomba mwenyekiti wake, Jaji Semistocles Kaijage kuiandikia barua Serikali ili kukomesha mchezo huo ambao alidai unatumia rasilimali nyingi za Taifa.

“Madiwani hao wanaonyesha kuwadharau wananchi na kuchezea rasilimali za nchi hii. Wananchi waamke, wasiwapigie kura madiwani hao kwa sababu wamewadharau,” alisema Muabhi.

Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa mchezo unaofanyika unafahamika na si kwamba unaua demokrasia pekee, bali pia hautendi haki kwa watu wengine ambao wana sifa na uwezo wa kuwa viongozi bora katika jamii zao.

Makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema suala hilo limechochewa zaidi na masilahi binafsi.

Alisema hali hiyo ikiendelea, Bunge lijalo la mwaka 2020 linaweza kuwa na wabunge wa upinzani wasiozidi 10.

Alisisitiza kwamba kinachofanyika kwenye chaguzi za sasa ni kutangaza washindi na siyo kuhesabu kura zilizopigwa.

“Siku hizi hakuna kuhesabu kura, kuna kutangaza mshindi. Niliwaambia wenzangu wakati wa uchaguzi wa Kinondoni kwamba tutashinda, lakini hawatatutangaza. Hata tukienda huko Buyungu, tutashinda lakini hawatatutangaza,” alisema.

Profesa Safari alisema sasa ni wakati wa kushinikiza kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi ili kusimamia demokrasia ya kweli na kuhakikisha mgombea aliyechaguliwa na wananchi ndiye anatangazwa kuwa kiongozi wa sehemu husika.

Madiwani waliopitishwa

Katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, madiwani wote wanne waliojiuzulu Chadema wamepitishwa na CCM kuwania udiwani.

Prosper Msoffe ambaye amewahi kuwa naibu meya wa jiji hilo amepitishwa kuwania udiwani Kata ya Darajambili. Wengine ni Elirehema Nnko (Osunyai), Obed Men’goriki (Terati) na Emmanuel Kessy (Kaloleni).

Wengine ni Bariki Sumuni (Monduli), Solomon Mollel (Lolkisale), Edward Mbapai (Naalarami), Benedict Mawala (Migungani), Emanuel Mtui (Engutoto), Loth Tarakwa (Meserani), Elias Mbao (Kamwanga), Lomayani Laizer (Olmolog), Jackob Mollel (Elang’atadapash), Lomayani Laizer (Olmolog) na Jackob Mollel (Elang’atadapash).

Kata ya Baray iliyopo wilayani Karatu ndiyo pekee ambayo CCM imesimamisha mgombea ambaye hakutoka Chadema kutokana na aliyekuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya Chadema, Moshi Darabe kufariki dunia. CCM imempitisha Elitumaini Magnus kuwania udiwani katika kata hiyo.

Katika Wilaya ya Ngorongoro yenye kata tano, wagombea wote walipita bila kupingwa.

Wagombea hao ni Daniel Orkeri (Ngorongoro), Lazaro Saitoti (Ngoile), Joseph Seuri (Pinyinyi), Boniface Kanjwel (Soitsambu) na Sokoine Moir (Alaitole).

Katika wWilaya ya Meru yenye kata moja ya Songolo CCM imempitisha Charles Nnko.

Mkoani Manyara waliopitishwa ni Nicodemus Tlaghasi (Bagara), Justin Masuja (Hayderer) na Paul Aweso (Tumati). Wengine ni Marco Martin (Masakta) na Mathayo Semhanda (Gehandu) ambaye alikuwa diwani kupitia ACT.

Chadema wanena

Akizungumzia hali hiyo mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema mpaka sasa chama hicho kimepoteza madiwani 50.

“Hatuna shida sisi. Kuhama kwao kunadhihirisha kile tulichokuwa tunakisema kuwa wanapewa rushwa, rushwa yenyewe ndiyo hiyo ya kupitishwa kuwania tena udiwani,” alisema.

“Pili, wasidhani kuwa wananchi wa Arusha watakuwa na sababu zilezile za kuwachagua kama walivyofanya walivyokuwa Chadema. Wananchi hawawezi kubadili uamuzi. Ila watambue kuwa na sisi Chadema tumejipanga.”

Wengine waanguka

Wakati Arusha mambo yakiwa mazuri, hali ni tofauti kwa Michael Kunani ambaye alikuwa diwani wa Kata ya Ikoma kwa tiketi ya Chadema. Kata hiyo ipo wilayani Serengeti Mkoa wa Mara.

Kunani ambaye alijiunga na CCM, ameanguka katika kura ya maoni ya chama hicho ambacho kimempitisha Moses Nguhecha aliyepata kura 18. Kunani aliambulia kura 17.

Mbali na Kunani, Joseph Mongita ambaye alikuwa diwani wa Kata ya Manchira kwa tiketi ya Chadema kabla ya kuhamia CCM, hakujitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.

Hata hivyo majina hayo yote yanasubiri baraka za kamati ya siasa wilaya na halmashauri ya chama hicho ngazi ya mkoa ili kupitisha jina la mgombea atakayepambana na vyama vingine.

Imeandikwa na Peter Elias, Joseph Lyimo, Musa Juma na Anthony Mayunga

Chanzo: mwananchi.co.tz