Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema kuipinga sheria ya utakatishaji fedha

90406 Chadema+pic Chadema kuipinga sheria ya utakatishaji fedha

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Uongozi wa Kanda ya Pwani ya Chadema umesema umeandaa mawakili wawili watakaofungua shauri mahakamani kupinga Sheria ya Makosa ya Utakatishaji Fedha Haramu, wakidai imekuwa ikitumika vibaya.

Utakatishaji fedha ni kitendo kuiingiza fedha haramu katika mzunguko wa pesa kwa kununua biashara halali, kujenga nyumba au kuweka kwenye benki, na watu kadhaa wameshtakiwa kwa kosa hilo, tukio la hivi karibuni likiwa la daktari aliyeshtakiwa kwa kutakatisha Sh250,000.

Jana, makamu mwenyekiti wa kanda hiyo, Baraka Mwago aliwaambia waandishi kuwa kimsingi makosa ya sheria hiyo hayana dhamana, lakini kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya watu kubambikiwa kesi.

“Kuna watu wamelalamika kuonewa kwa kushitakiwa kwa makosa ya sheria hiyo,” alieleza Mwago.

“Kuna malalamiko ya mtu kukamatwa na kosa fulani lakini akifika mahakamani anaambiwa anashtakiwa kwa utakatishaji fedha.”

Mwago alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa tathmini ya masuala mbalimbali, yakiwamo ya kiuchumi na siasa yaliyojitokeza katika kipindi cha Januari hadi Desemba.

Kwa mujibu wa Mwago, huenda idadi ya mawakili watakaotumwa na chama chake kwenda mahakamani ikaongezeka kulingana na mahitaji huku akibainisha kuwa mchakato utafanyika mapema mwakani baada ya shughuli za mahakama kuanza.

“Natoa wito kwa wananchi, taasisi, mashirika ya ndani na nje ya nchi tuungane kwa pamoja kuipinga sheria hii kandamizi. Tuikemee ili watu wasionewe kupitia sheria ya utakatishaji fedha,” alisema Mwago.

Alisema kuna baadhi ya watu wakiwemo wanaharakati wamekumbana na sheria hiyo na kujikuta wakikaa mahabusu kwa muda mrefu bila kupata dhamana.

Alipoulizwa uwezekano wa jambo hilo kufanikiwa, wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole aliiambia Mwananchi kuwa ni uamuzi mzuri wa Chadema kwa sababu wametumia haki yao ya kikatiba akisema hatua hiyo inaweza kusaidia kuondoa utata wa sheria hiyo katika suala la dhamana.

“Kila kosa linapaswa kuwa na dhamana, lakini sheria hii haitoi dhamana. Hii ni kinyume cha haki za binadamu,” alisema Kambole.

Alisema kinachotakiwa katika sheria hiyo ni kuwekwa masharti ya dhamana yatakayombana mshtakiwa kuhudhuria mahakamani kila anapohitajika.

Wakili mwingine wa Tume ya Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe aliungana na Kambole akisema ni hatua nzuri kama Chadema watakwenda mahakamani kuipinga sheria hiyo.

Alisema mfumo unaruhusu kila mtu kwenda mahakamani kupata tafsiri sahihi ya sheria kama ina ukakasi.

“Tatizo lililopo ni namna sheria hii ya utakatishaji fedha inavyotumika,” alisema Massawe.

“Sheria inataka mtu apelelezwe ndipo akamatwe. Lakini sasa hivi unakamatwa halafu upepelezi unafanyika, jambo ambalo ni kinyume na tafsiri yake.”

Katika mkutano huo, Mwago pia alizungumzia usafiri wa mwendokasi akisema umekuwa kero na kushauri mabasi takriban 70 yaliyozuiwa bandarini yatolewe ili kupunguza matatizo.

“Magari yaliyopo hayatoshi,” alisema. “Kwa nyakati tofauti ndani ya mwaka huu tumeshuhudia msongamano wa abiria kwenye vituo vya mabasi.”

Chanzo: mwananchi.co.tz