Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema inahitaji kipaumbele cha ziada kupigania Tume Huru ya Uchaguzi

90265 Chademaa+pic Chadema inahitaji kipaumbele cha ziada kupigania Tume Huru ya Uchaguzi

Mon, 30 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Chadema imemaliza mkutano wake mkuu ikipata safu mpya ya uongozi na ikijiwekea malengo manono kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020.

Licha ya Freeman Mbowe kuchaguliwa tena kwa kishindo kuendelea na uenyekiti wa chama hicho, safu ya uongozi iliyowekwa imetajwa kulenga kukabiliana na mikikimikiki ya siasa za utawala wa awamu ya tano na kuelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.

Uteuzi wa John Manyika, mbunge wa Kibamba kuwa Katibu mkuu wa chama hicho, akimrithi Dk Vincent Mashinji kunatajwa kuwa kimkakati wa kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho.

Mnyika atasaidiana na Singo Benson Kigaila aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu mkuu Bara akichukua nafasi iliyoachwa na Mnyika huku Salum Mwalimu akiendelea na nafasi yake ya Naibu katibu mkuu Zanzibar.

Mbali na uteuzi huo, Tundu Lissu, mbunge wa zamani wa Singida Mashariki amechaguliwa akiwa nje ya nchi na mkutano huo kuwa makamu mwenyekiti Bara na Issa Mohamed Issa kushika nafasi kama hiyo Zanzibar.

Safu hiyo imekuja wakati Chadema na vyama vingine vya upinzani vikikabiliwa na changamoto kubwa za kisheria ikiwa pamoja Serikali kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano.

Tayari mtendaji mkuu wa Chadema, John Mnyika ameainisha vipaumbele vitano vya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ikiwa pamoja na kudai Tume Huru ya Uchaguzi.

Kipaumbele cha pili ni maandalizi ya wagombea kuelekea uchaguzi mkuu, tatu ni kuandaa ilani ya uchaguzi ya chama hicho, nne ni kuendeleza sera ya ‘Chadema ni Msingi’ na tano kuendeleza Chadema Digitali.

Huku akiwashukuru wanachama waliopokea vyema uteuzi wake, Mnyika amesema, “kazi kubwa ya chama cha siasa ni kushika dola, hili ndiyo lipo mbele yetu kwenye uchaguzi wa mwakani.”

Anasema katika mkakati huo vipaumbele hivyo “vitatekelezwa kwa ufanisi na Watanzania watarajie mabadiliko.”

Mnyika anayasema hayo wakati chama hicho kikijitutumua kukusanya wanachama wapya zaidi ya milioni sita waliotokana na kazi ya Chadema ni Msingi iliyofanyika ndani ya miezi 20.

Pamoja na mikakati hiyo, wachambuzi wa hali ya kisiasa wanaona changamoto kubwa inayoikabili Chadema ni kutokuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na huenda maandalizi yote ya uchaguzi wa 2020 yakaishia kupoteza kama ilivyotokea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo CCM ilishinda kwa zaidi ya asilimia 99.

Suala la kuwa na Tume huru ni mjadala wa muda mrefu kutokana na madai ya Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kuongozwa na baadhi ya makada wa CCM jambo linalotishia uhuru wake.

Uteuzi wa Dk Wilson Mahera Charles kuwa Mkurugenzi wa NEC, ulizua mjadala mkali baada ya baadhi ya wadau kulalamika kuwa amewahi kugombea nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu ya CCM kupitia Mkoa wa Mara.

Hata hivyo, Dk Mahera aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha amewahi kukanusha madai hayo alipozungumza na baadhi ya waandishi wa habari.

Mbali na Dk Mahera, uteuzi wa Omari Mapuri kuwa kamishna wa NEC unazidisha utata. Huyo amewahi kushika idara ya uenezi ya CCM, Suala hilo sasa limefikishwa mahakamani na Wakili wa kujitegemea Alex Masaba akipinga uteuzi wa Dk Wilson Mahera na Mapuri.

Katika kesi hiyo namba 30 ya mwaka 2019, wakili Masaba ambaye anajiwakilisha mwenyewe, anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa uteuzi huo ni batili kwa kukiuka na kuvunja masharti ya Katiba.

Pia anaomba mahakama itamke kuwa wateule hao wameshindwa kuzingatia wajibu wao wa masharti ya Katiba kwa kukubali uteuzi huo kwani kwa mujibu wa Ibara ya 26(1) (2) kila raia anawajibu wa kuzingatia kulinda na kuhifadhi Katiba na sheria za Tanzania.

Pamoja na njia hiyo, wachambuzi bado wanaona njia ya mahakama ina miiba mingi na si rahisi kuipitia na kufikia Tume Huru ya Uchaguzi.

Mwanasheria maarufu, Fatma Karume aliyekuwa akisimamia kesi ya kupinga wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi iliyofunguliwa na Bob Wangwe, anailaumu Mahakama ya Rufaa kwa kutupilia mbali uamuzi wa Mahakama Kuu katika suala hilo.

“Mahakama Kuu iliona kuna tatizo na ikajaribu kusuluhisha, Mahakama ya Rufaa ikaja ikapuuza. Kwa hiyo mimi nilishafanya wajibu wangu kama mwanasheria, yanayofuata ni kwa wananchi wenyewe,” anasema Karume.

Kwa maoni yake, mwanasheria huyo anaona Tanzania iko kwenye janga la kisiasa, huku akirejea uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka huu.

Hata Bob Wangwe ambaye ni mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania, anasema kwa sasa hakuna matumaini ya kupata Tume Huru ya Uchaguzi kwa njia ya mahakama.

Hivyo, Wangwe anaishauri Chadema iwe na kipaumbele cha ziada, yaani ihamasishe umoja wa kitaifa kwa kuungana na vyama vingine na taasisi nyingine ili kuweka msukumo wa pamoja wa kudai Tume Huru ya Uchaguzi.

“Watafute njia yoyote itakayoleta msukumo wa pamoja. Waunganishe vyama vya siasa vyote 18, asasi za kiraia na makundi mengine ili kuwe na msukumo wa pamoja wa kudai Tume Huru ya Uchaguzi,” anasema.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Profesa wa Sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha Iringa, Gaudence Mpangala akisema Chadema peke yake haitaweza kudai Tume huru ya uchaguzi.

“Lazima kuwe na muungano wa vyama vya siasa na makundi mengine ili kuwe na msukumo wa pamoja. Bila hivyo hawawezi kushinda uchaguzi wowote iwe ni wa udiwani, ubunge wala urais,” anasema Profesa Mpangala.

Ameongeza, “Vyama vya siasa viungane vipeleke msukumo wa pamoja, ikiwezekana vihusishe asasi za kiraia na jumuiya za kimataifa za haki za binadamu bila kuwaacha viongozi wa dini.”

Mipango mingine

Pamoja na ushauri huo, Chadema inayo mipango yake ambayo inaamini itaiwezesha kuwa na nguvu na ushindani wa kutosha katika uchaguzi mkuu.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa Chadema hivi karibuni, Mwenyekiti wa chama hiyo, Freeman Mbowe anasema moja ya njia hizo ni kujiimarisha kiuchumi kwa kutumia rasilimali watu ambao ni wanachama.

Anasema katika mkakati huo ni Chadema ni Msingi alioamua ufanyike licha ya wasiwasi wa baadhi ya viongozi.

“Nikawaambia viongozi wangu kama huko chini kuna wananchi wanaishi na sisi tutakwenda kuishi nao. Kama wanalalia virago na sisi tutalalia virago na hili zoezi mimi kama mwenyekiti wa Taifa nitalisimamia mwenyewe bila kufuata mfumo wowote wa kichama.”

Kutokana na mkakati huo, anasema zaidi ya asilimia 70 ya wajumbe waliohudhuria mkutano mkuu wanatokana na Chadema ni Msingi.

Kutokana na mafanikio hayo, anasema chama hicho kimeandaa orodha ya wanachama wake itakayokuwa ya kidigitali na wanachama hao watakuwa wakichangia chama hicho ada ya Sh2,500 kwa mwaka.

Kwa kiwango hicho, Mbowe amesema chama kinatarajia kukusanya Sh15 bilioni kwa mwaka na kuwa uhakika wa kujiendesha bila kutegemea ruzuku ya Serikali.

Chanzo: mwananchi.co.tz