Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema haina mpango wa kususia uchaguzi wowote

13409 CHADEMA+PIC TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chadema imesema itaendelea kushiriki uchaguzi licha ya changamoto zilizopo na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe amesema kususia ni sawa na kukubali kukipa ushindi chama tawala.

Mbali ya Mbowe, msimamo huo pia umetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.

Mbowe ambalisema hayo juzi baada ya kuulizwa na mwandishi wetu msimamo wake kuhusu Chadema kushiriki uchaguzi baada ya Agosti 18, makamu mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Profesa Abdallah Safari kushauri kisusie chaguzi zote nchini ikiwa ni njia mojawapo ya kudai tume huru ya uchaguzi.

Mbowe alisema hata ndani ya Chadema na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wapo wanaotaka wapinzani kususia uchaguzi kwa sababu ya ukiukwaji wa demokrasia.

“Wapo wanachama wanaosema ukimsusia asiyejali demokrasia kwake ni kicheko. Wapo wanaotaka tushiriki uchaguzi na wapo wanaotaka tusishiriki, hii ipo ndani ya Chadema na hata ndani ya Ukawa,” alisema.

“Ninaheshimu mawazo ya Profesa Safari ni hisia kama za wengine kwamba hatutendewi haki. Hata mimi ninaweza kupinga jambo ila maamuzi ya vikao ni wengi wape,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, alisema ni lazima kushiriki uchaguzi kwa kuwa katika kampeni ndiyo sehemu pekee ya kufikisha ujumbe kwa hali ilivyo sasa.

Profesa Safari alitoa kauli ya kususia uchaguzi wakati Chadema ikiugulia maumivu ya kupoteza Jimbo la Buyungu.

Jimbo hilo lilikuwa chini ya Chadema mbunge akiwa Kasuku Bilago. Baada ya kifo chake na uchaguzi kufanyika Agosti 12 sasa lipo mikononi mwa CCM baada Christopher Chiza kuibuka mshindi.

Chadema na vyama vingine vya upinzani pia vimepoteza kata 77 za udiwani baada ya CCM kuibuka na ushindi.

Uchaguzi huo uliibua malalamiko na hivi karibuni ubalozi wa Marekani nchini ulitoa tamko ukidai kulikuwa na ukiukaji wa sheria ikiwa ni pamoja na baadhi ya watendaji wa NEC kukataa kuwasajili wagombea kutoka vyama vya upinzani.

Ubalozi huo pia ulidai kulikuwa na vitisho vya polisi dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani, watu kukamatwa bila kuwapo vibali vya ukamataji na kukandamizwa kwa uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni katika kipindi cha kuelekea uchaguzi.

NEC iliujibu ubalozi huo ikiutaka kudhibitisha ilichokieleza juu ya uchaguzi huo, ikisema huwa hauna waangalizi wa kimataifa, hivyo kuhoji ni wapi ulipata taarifa hizo.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kuufahamisha umma kuwa Tanzania ni nchi huru na inaendesha chaguzi zake kwa mujibu wa Katiba yake na sheria za uchaguzi,” ilisema NEC katika taarifa yake.

Mbowe akizungumzia ushiriki wa chama hicho katika uchaguzi alisema, “Katika kampeni watu watazungumza na kueleza mambo mbalimbali na kwa watakayoyaeleza hata kama hatutashinda, ujumbe utakuwa umefika na kutua katika mioyo ya wananchi, hata nje ya nchi.”

Alisema kutoshiriki uchaguzi ni sawa na kuwaumiza wapenda demokrasia, wafuasi na wanachama wa Chadema na vyama vya upinzani.

Mbowe alisema kushiriki kwao uchaguzi kunawafanya wananchi kuelewa kinachoendelea na kujipanga kwa yajayo.

Akizungumzia kuhusu wagombea wa Chadema kuenguliwa kutokana na sababu mbalimbali zinazotolewa na wasimamizi wa uchaguzi, akitoa mfano wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Mbowe alisema, “Kama wanajiamini Korogwe ni yao waache twende katika uchaguzi waone.”

Alisema katika uchaguzi, wagombea wanapaswa kuachwa wanadi sera kisha wananchi wapige kura kumchagua mgombea wanayemtaka na si vinginevyo.

Katika Jimbo la Korogwe Vijijini, mgombea wa CCM Timotheo Mzava ametangazwa kupita bila kupingwa ikielezwa ndiye pekee aliyerejesha fomu.

Chadema inadai mgombea wake, Amina Saguti hakurejesha fomu kutokana na msimamizi wa uchaguzi kutokuwapo ofisini.

Kauli ya Lissu

Mbali ya Mbowe, mwingine aliyezungumzia suala la ushiriki wa Chadema katika uchaguzi ni Lissu. Akizungumzia kilichojitokeza Korogwe Vijijini alisema ameshuhudia ‘utoto’ wa kisiasa.

“Licha ya haya yote, hatukuwahi kufikiria kuacha kushiriki kwenye chaguzi za marudio au uchaguzi mkuu,” alisema Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki.

“Tulijua uchaguzi ni vita na vitani kuna kushinda au kushindwa; kuna kufa au kujeruhiwa au kutekwa na kuna kuua au kujeruhi au kuteka,” alisema.

Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu alisema, ‘marafiki’ waliokuja jana na leo asubuhi wameshuhudia wakipigwa na sasa tayari wanatushauri tunyanyue mikono juu na kusalimu amri mbele ya watesi wetu.

“Wanatushauri tususie chaguzi zijazo ili CCM ipite bila kupingwa kwenye nafasi zote nchi nzima. Wanatumia maneno makali yenye kuonyesha wana msimamo mkali na ujasiri ambao hatujawahi kuona wakiuonyesha kwa vitendo mahali popote,” alisema.

Lissu alipoulizwa iwapo ujumbe wake unalenga alichozungumza Profesa Safari alisema, “Hapana, wala sikuwa nimesikia ushauri wa Profesa Safari. Nilikuwa nawasema hao waliokuwa wanazungumza hiyo habari (ya Korogwe Vijijini).”

Lissu anayeendelea na matibabu baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 mwaka jana akiwa Dodoma alisema kinachopaswa kufanyika ni kujielewa na kuelewa, “Tunaelewa hali yetu ya sasa kwa sababu kila mmoja wetu anaona yanayotendeka. Hata hivyo, uelewa wetu wa sasa hautoshi kututabiria kesho yetu. Ili tuelewe kesho yetu itakuwaje ni lazima tuelewe jana na juzi yetu ilikuwaje.”

Lissu alisema, “Tusikubali ujasiri feki na ushauri wa sumu wa hawa wanaojiita ‘marafiki’ zetu. Tusikubali kutengenezewa ugomvi wa bure baina yetu na viongozi wetu na hawa wanaojifanya wana uchungu na chama.”

“Tusikubali kupotezewa malengo kwa kuaminishwa kuwa adui ni (Freeman) Mbowe au (Dk Vincent) Mashinji au (John) Mnyika; wakati adui halisi ni yule aliyemuua (aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, Geita- Alphonce) Mawazo na kumpoteza Ben Saanane au kumjeruhi Tundu Lissu,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz