Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema chapata wagombea ubunge Morogoro

81a00fd69a1aa99d08c26f634fb1b3a2.png Chadema chapata wagombea ubunge Morogoro

Mon, 20 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Morogoro kimeendelea na mchakato kupiga kura za maoni nafasi ya ubunge kwenye majimbo 11 mkoani humo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Morogoro , Jackson Malisa alisema jana kura za maoni Jimbo la Mikumi mgombea pekee ni Mbunge aliyemaliza muda, Joseph Haule (Profesa Jay).

Katika uchaguzi huo wapiga kura walikuwa ni 138, Profesa Jay alipata kura za ndiyo 137, kura moja iliharibika na hakukuwa na hapana. Jimbo la Mlimba wagombea walikuwa wawili akiwemo Mbunge aliyemaliza muda aliyeshinda kwa kura 88 dhidi ya 33 za Haji Kidinya. Kwa Jimbo la Morogoro Mjini aliyekuwa Mbunge wa Viti maalumu, Devotha Minja alishinda kwa kura 83 dhidi ya watatu.

Jimbo la Malinyi lilikuwa na wagombea watatu, mshindi alikuwa ni Imelda Maley. Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, alijitokeza mgombea Onesfori Mbuya na kupigiwa kura za ndiyo 45 kati ya kura zote 47 , kura moja ya hapana na moja iliharibika.

Kwa Jimbo la Ulanga wagombea walikuwa ni Selestine Simba aliyeibuka mshindi kwa kura 60, Jimbo la Kilombero wagombea walikuwa sita na Modestus Chitemi akashinda kura 107.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chadema mkoa huo, uchaguzi huo utaendelea kwa jimbo la Kilosa, Mvomero, Gairo na Morogoro Kusini. Wakati huo huo, Chama cha Wananchi CUF Wilaya ya Morogoro mjini kupitia Mwenyekiti wake, Abeid Mlapakolo kinatarajia kufanya Mkutano Mkuu kesho kuchagua wagombea wake ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini.

Chanzo: habarileo.co.tz