Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema Ukonga wawataka wananchi wasisusie uchaguzi

14579 Pic+ukonga TanzaniaWeb

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wananchi wa Ukonga wameombwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Septemba 16, 2018 ili wasipoteze haki zao kwa kuususia uchaguzi huo.

Hayo yamesemwa leo jioni Agosti 29 na Diwani wa Majohe, Waziri Malijale katika mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa ubunge wa Ukonga wa Chadema uliofanyika viwanja vya Italiani vilivyopo Buyuni, Chanika.

“Niwaambie wana Buyuni na Ukonga kwa ujumla msisusie kwenda kupiga kura mkifanya hivyo ni kuwapa mafanikio msiowapenda,” amesema Malijale.

Amesema kuna watu wanazunguka mtaani kununua shahada hivyo amewataka wananchi wasihadaike, “Ukiona mtu kama huyo ni mwizi mkamateni na kumfikisha eneo husika ni wizi na kosa kisheria.”

Naye Mkuu wa Idara ya Usalama na Ukufunzi wa Chadema, Benson Kigaia amesema chama hicho kimefanya chaguzi ndogo kwenye majimbo kadhaa kwa sababu wabunge walipata matatizo wengine kufariki lakini si kwa jimbo la Ukonga hivyo mgombea wa CCM Mwita Waitara anachezea fedha za wananchi.

“Tulifanya uchaguzi majimbo kadhaa sababu wanachadema kama Chacha Wangwe walifariki, lakini leo hii tuliyemhangaikia tukalinda kura akatangazwa akashinda na kuingia bungeni ameuacha bila sababu halafu anarudi tena hii si sawa.

“Ni sawasawa na mtu wa dini anakaa kwenye dini yake anaasi kisha anarudi kanisani au msikitini hayupo sawa, hamuwezi kuwa na kazi ya kumchagua Waitara kwenye jimbo la Ukonga kila siku, kama aliuchoka ubunge akae pembeni aingie mwingine naye ni Asia Msangi,” amesema Kigaia.

Wakati akiomba kura, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Asia Msangi amesema yeye ni mbunge atakayekwenda kuwaunganisha watu wa makundi mbalimbali kwenye jamii pasina kuwabagua.

“Msiogope hali ni mbaya kisiasa lakini msiogope tokeni mkapige kura,” amesema Asia

“Nilipambana kabla ya kuwa mbunge, niliwaletea mikopo midogo midogo naomba niwaambie mama hakimbii familia, nawaambia nitapambana mpaka mwisho nawaambia msiogope tuuvae ujasiri tulipiganie taifa,” amesema Asia.

Asia amesema akiwa mbunge atakuwa tayari kupokea mawazo ya kila mmoja.

Akigusia vijana amesema, “Mimi mwanamke nanyi ni vijana nitaanzisha ligi mbalimbali jimbo la Ukonga, nitageuza michezo kuwa ajira jimbo la Ukonga.”

Kuhusu fedha za mfuko wa jimbo, Asia amesema: “Pesa ya mfuko wa jimbo, kuna pesa huwa inaingia lakini waliopita walikuwa wanauficha, mimi ni mbunge nitakayeweka mambo wazi kiasi gani kimeingia na kipi kimetumika, lazima pesa za wananchi wa Ukonga ziwekwe wazi zijulikane.”

Chanzo: mwananchi.co.tz