Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema: Tumejitofautisha, wataiga hawataweza kutekeleza

Mon, 1 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kipengele namba moja katika sera mpya za Chadema ni Katiba Mpya. Bila shaka kipengele hiki kimewekwa kimkakati katika nafasi hiyo kwa kuwa ni kipaumbele chake – Katiba ni mwongozo wa namna kila kitu kitakavyokwenda endapo chama hicho kitakabidhiwa nafasi ya kuongoza nchi.

Katika kitabu cha kurasa 81 cha sera hizo, imewekwa bayana kwamba endapo Chadema itapewa ridhaa ya kuongoza, “Itahakikisha kwamba nchi inapata Katiba Mpya itakayotokana na maoni ya wananchi.”

Pengine suala la Katiba ambalo pamoja na mambo mengine linabeba hoja muhimu za haki za binadamu, uhuru wa kujieleza, mfumo wa utoaji haki na utawala wa sheria, ndilo linaloweza kuwa msingi wa tofauti kati ya sera za Chadema na vyama vingine, hasa chama tawala, CCM.

CCM ambayo sera yake kwa kiwango kikubwa inaweza tu kutazamwa kupitia mambo yanayoendelea kutekelezwa na serikali, mwaka 2015 iliahidi kukamilisha mchakato wa kutunga Katiba Mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kuendeleza utawala bora, demokrasia na uwajibikaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo (Ilani 2015-2020).

Bila shaka kwa sasa chama hicho kitakuwa kinasubiria uamuzi wa mwenyekiti wake, Rais John Magufuli aliyekwishasema kuwa kwa sasa Katiba si kipaumbele chake.

Katiba mpya inayotajwa na CCM katika ilani ni Katiba Inayopendekezwa, ambayo mchakato wake ulikumbana na malalamiko na mgawanyiko katika Bunge Maalumu la Katiba, ikidaiwa kuwa maoni mengi ya wananchi yaliondolewa.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa CCM hicho, Chadema inasema Katiba mpya lazima itokane na maoni na mapendekezo ya wananchi juu ya namna wanavyotaka wajitawale na namna wanavyotaka dola pamoja na taasisi, na mashirika mengine yaendeshwe.

“Katiba itakuwa na uhalali pale tu matakwa ya wananchi yatakapoheshimiwa katika nyanja zote za maisha,” inasema sera hiyo ya Chadema.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anasema Katiba Mpya inayokusudiwa kutungwa chini ya Chadema itaweka misingi na kutamka kinagaubaga juu ya mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mikuu ya dola na pia kuweka misingi ya kudhibitiana baina ya mihimili hiyo ili kulinda haki za binadamu.

Katika eneo la haki za binadamu, sera hiyo ya Chadema imezama zaidi ikitanabahisha kwamba ikichukua madaraka ya kuongoza dola, itaridhia sheria za kimataifa za haki za binadamu, kutunga sheria zinazolinda haki za binadamu na kuzitekeleza, kufanya marekebisho au kufuta sheria zinazokandamiza haki za binadamu, kuhamasisha na kutoa elimu ya uraia juu ya haki za binadamu na kuanzisha vyombo vya kusimamia haki za binadamu.

Lengo la kufanya hayo yote, Mbowe anasema ni kuona jamii huru yenye kutenda haki, ambayo inaheshimu na kufuata misingi ya haki za binadamu ambapo demokrasia na utawala bora vinaheshimiwa.

Ili kufikia hali hiyo, chama hicho kinasema kitahakikisha sheria zote zinazokandamiza haki za binadamu “zinafutwa bila kuchelewa na kuanzisha vyombo madhubuti vya kusimamia haki za binadamu”.

Katika kipengele kingine cha Katiba Mpya, chama hicho kinazungumzia uhuru thabiti wa kujieleza, kwamba kitatoa uhuru wa kujieleza, uhuru wa habari na vyombo vya habari na kufuta sheria kandamizi za uhuru wa habari.

Katika hatua hiyo, kusudio la Chadema ni kufuta na kutunga upya sheria ya makosa ya kimtandao, sheria ya takwimu, na sheria ya huduma za vyombo vya habari ambazo chama hicho kinasema zimekuwa kikwazo cha kuwa na jamii huru kupata, kutumia na kutoa habari.

Ukiacha eneo la uhuru wa kujieleza, sera hiyo imeibua hoja nzito katika mfumo wa utoaji haki ambao chama hicho kinautaka, kikianza na uhuru wa Mahakama, kuwa na chombo cha kusimamia utekelezaji wa sheria kinachozingatia utawala wa sheria na kupanua Mamlaka ya Mahakama ya Katiba.

Katika eneo hilo, Chadema inasema inataka taratibu za utoaji haki zifuatwe na kuzingatiwa kuanzia kwenye vituo vya polisi, mahakama na magereza na kuhakikisha amri za mahakama zinatekelezwa.

Kuhusu utawala wa sheria, sera hiyo inasisitiza kuwa katika nchi hakuna aliye juu ya sheria na hivyo kila mtu, watumishi wa umma, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi waliochaguliwa, majaji na mahakimu wote wanastahili kufuata sheria.

Ugatuaji madaraka

Eneo la pili ambalo Chadema imelipa kipaumbele katika ilani yake ni Utawala Bora. Hili linabeba uwazi na uwajibikaji, mapambano dhidi ya rushwa, ushirikishaji wa wananchi kulinda demokrasia na kuwa na viongozi waliochaguliwa na wananchi na taasisi huru za uchaguzi.

Katika eneo hili ambalo pia linazungumzia Muungano, pia ipo tofauti ya wazi kati ya sera ya Chadema na mfumo uliopo sasa, ambao inaaminika ndiyo sera ya chama kinachotawala.

Matokeo ya sera hii ya utawala bora ndipo linajitokeza suala la utawala wa majimbo, chama hicho kikiwa kimeigawa nchi katika majimbo 10, manane bara na mawili Zanzibar. Chini ya mfumo huo, viongozi wa majimbo watachaguliwa na wananchi na kufuta mfumo wa sasa wa wakuu wa wilaya mikoa ambayo wanateuliwa na Rais.

Chama hicho kinakusudia kurejesha madaraka kwa wananchi katika Serikali za shirikisho zilizochaguliwa na wananchi, kugatua madaraka ya taasisi za Serikali Kuu kwenda kwenye serikali za ngazi ya majimbo na mitaa.

Ili kufanikisha hilo, Chadema inadai itahakikisha madaraka ya Serikali yanatokana na wananchi, mapato ya Serikali yanabaki kwa wingi zaidi katika maeneo yanakokusanywa na kuwapo mamlaka kamili katika ngazi zote za utawala.

Malengo ya sera hii ni chama hicho kutaka kuona uwazi serikalini ambapo wananchi watakuwa na haki ya kujulishwa kila hatua ya shughuli za Serikali na kuwa na uwezo wa kuhoji kila ambacho Serikali inafanya.

“Chadema inataka kuona nchi yenye taasisi huru za uchaguzi ambazo zitakuwa ni vyombo pekee ya kusimamia uchaguzi...Ugatuaji wa namna hii unahitaji kuwa na viwango vya hali ya juu vya uadilifu katika utekelezaji majukumu ya umma,” inasema sehemu ya ilani hiyo.

Tofauti na Chadema utaratibu wa sasa wa serikali ya CCM ni Rais kuteua wakuu wa wilaya, maofisa tawala na wakurugenzi wa wilaya; vivyo hivyo wakuu wa mikoa na maofisa tawala wa mikoa. Rais anateua pia wakurugenzi wa mashirika mbalimbali, mawaziri, naibu mawaziri, wenyeviti wa bodi za mashirika, mabalozi na majaji, nafasi ambazo wapinzani na hasa Chadema, wamekuwa wakisema ni madaraka makubwa mno.

Kuhusu muungano, Chadema inalenga mambo makuu matatu, kuboresha muundo wa muungano, kufafanua mambo ya muungano na kukusa mamlaka ya nchi juu ya rasilimali.

Sera hiyo ambayo haitofautiani sana na ilani ya chama hicho, inasema inakusudia kujenga muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao unadumisha Serikali tatu; Serikali ya Shirikisho ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar; Muungano wenye uhalisia na uwazi kuhusu mambo ya muungano.

“Chadema inataka masuala ya msingi ya jumla yashughulikiwe na Serikali ya Shirikisho ya Jamhuri ya Muungano. Mambo hayo ni katiba ya shirikisho, mambo ya nje, ulinzi na usalama, uraia, sarafu na Benki Kuu, Mfumo wa elimu, Mahakama ya Katiba, na Bunge la shirikisho, Inasema sera hiyo.

Sera hiyo inasema kuwa Chadema itajenga mamlaka ya nchi ya kila mshirika wa Muungano katika kumiliki na kutumia rasilimali na maliasili zake.

Chini ya mfumo huo, Chadema inaamini wananchi watanufaika kwa kuwa kutakuwa na matumizi makini ya rasilimali za nchi na Muungano utaimarika.

Maeneo mengine

Sera hiyo inazungumzia maeneo mengine ambayo pia Chama tawala kinayo lakini yanatekelezwa kwa njia tofauti, uchumi wa soko jamii, ambao Chadema inasema ni ule unazingatia maendeleo ya jamii.

Uchumi huo ni wa kushirikisha sekta binafsi, huku chama hicho kikiweka mkakati jumuishi wa uchumi wa Taifa. Mkakati huo ni kuimarisha uchumi kukabiliana na changamoto za ajira na bei ya bidhaa, kuweka mfumo wa kodi unaoratibika, kuweka uwiano wa mauzo ya nje na bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi na kusimamia deni la Taifa ambalo linatajwa kukua kila mara.

Jambo jingine linalotajwa katika sera hiyo ni uchumi wa viwanda wenye tija na usimamizi wenye tija wa sekta ya madini.

“Lengo la eneo hilo ni kupinga dhana kuwa umasikini ni sifa. Watu wengi wanadhani umasikini ni sifa. Umasikini siyo sifa, ni laana. Sisi tunataka watu wote wawe matajiri,” anasema Mbowe katika uzinduzi huo.

Anasema baada ya kuhakikisha sekta binafsi inahusika kwa kiwango kikubwa kwenye uchumi. Serikali itaachiwa fursa ya kutoa huduma za jamii kwa wananchi kwa kuwa ndilo jukumu lake.

“Kumejengeka dhana kuwa huduma za kijamii kama hospitali, shule, zahanati zimejengwa na serikali ni kama msaada au ofa, kiuhalisia haya yote ni jukumu la Serikali,” anasema.

Baada ya kukamilisha hafla ya uzinduzi wa sera hiyo, mjumbe wa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye akatoa hisia kuhusu washindani wao.

Akasema, Chadema imefanya kama ambavyo Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, kuwa ni lazima chama cha siasa kuwaeleze wananchi namna kitakavyowaongoza.

“Na sisi ndivyo tulivyofanya. Najua kuna watu watakaozibeba hizi na kuzipinduapindua, lakini watazipapasa tu, hawatafanya kinachokusudiwa,” akasema Sumaye.

Kuhusu suala la kuiga sera hizo, Mbowe aliweka bayana kuwa watakaotaka kuzichukua wanakaribishwa lakini wasione haya kueleza kuwa wamechukua kwa chama hicho cha upinzani.

Chanzo: mwananchi.co.tz