Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema, Magereza wavutana kupigwa kwa kina Halima Mdee

99091 Pic+chadema+magereza

Mon, 16 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Magereza  Tanzania likisema lililazimika kutumia nguvu ya wastani kuwazuia wanachama na viongozi wa Chadema waliokuwa wanataka kuingia katika gereza la Segerea na magari, chama hicho kimedai taarifa hiyo inatetea uovu.

Taarifa hiyo ya Magereza iliyotolewa leo Jumamosi Machi 14, 2020 na msemaji wa jeshi hilo, Amina Kavirondo imekuja ikiwa imepita siku moja tangu wanachama 27 wa Chadema kushikiliwa na kuachiwa na polisi baada ya kupigwa na askari Magereza na baadhi yao wamelazwa katika Hospitali ya Aga Khan.

Kavirondo amedai wanachama hao waliingia katika eneo la kiusalama na kutoa maneno ya kashfa, vitisho na kumshambulia askari aliyekuwepo zamu na kumchania sare zake, kitendo kilichosababisha askari kufuata itifaki za kiusalama na kuwaondoa kwa nguvu ya wastani hadi nje ya Magereza.

Kwa mujibu wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, wanachama wake walipigwa walipofika katika gereza hilo kumchukua mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyekuwa akitoka jela baada ya kukamilisha taratibu za kulipa faini ya Sh70 milioni.

Baadhi ya waliopigwa ni  mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; mbunge wa Viti Maalum, Jesca Kishoa;  Meya wa Ubungo, Boniface Jacob; katibu wa Chadema Dar  es Salaam Kuu, Henry Kileo  na diwani wa Tabata, Patrick Assenga.

Taarifa hiyo ya Magereza imebainisha kuwa kwa mujibu wa sheria za Magereza ni mtu mmoja tu ndio anaruhusiwa kuingia kukamilisha taratibu za kumtoa mtu.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Kitendo cha viongozi hao na wafuasi wa Chadema ni kushindwa kutii sheria bila shuruti na kuhatarisha usalama wa wafungwa, askari na mali za jeshi la magereza,” imeeleza sehemu ya taarifa

Baada ya taarifa hiyo, Chadema kupitia kwa msemaji wake, Tumaini Makene ilitoa taarifa kulaani kilichoelezwa na Magereza.

Inaeleza kuwa Magereza wanajaribu kutetea au kuhalalisha vitendo vya kikatili, vinavyokiuka haki za binadamu na misingi ya sheria za nchi vilivyofanywa na askari wa jeshi hilo.

Chama hicho kimeutaka uongozi wa jeshi hilo kuchukua hatua kali dhidi ya askari waliohusika kufanya ukatili kwa wanachama na viongozi wao huku wakibainisha kuwa kukalia kimya na kutoa taarifa ya kuwatetea, ni kuanza hatua za kupoteza imani ya wananchi kwa chombo hicho.

“Hiyo ni kutokana na kile walichobainisha kuwa Jeshi la Magereza ni chombo cha dola kinachotakiwa kuonyesha mfano bora kwa kutekeleza majukumu yake kwa misingi ya sheria inayozingatia haki na kukataza upendeleo wa aina yoyote ile.”

“Tungependa jeshi hilo liendelee kupewa heshima inayotokana na utendaji kazi na umahiri wa askari na uongozi wa jeshi kusimamia shughuli zake bila kuwepo harufu ya ubaguzi wa aina yoyote ile, ukiwemo wa kisiasa, katika utoaji wa huduma na haki zinazotakiwa kutolewa na chombo hicho,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya Chadema.

Inaeleza, “Chadema inalaani na kupinga vikali vitendo walivyofanyiwa viongozi wake, wabunge, madiwani na wanachama kwa kukamatwa, kupigwa, kupewa mateso ya kutweza utu na heshima ya ubinadamu bila kosa lolote.”

Chanzo: mwananchi.co.tz