Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadema: Kuahirishwa kesi wanasogeza muda

Mdee Mahakamani Wenzake.jfif Chadema: Kuahirishwa kesi wanasogeza muda

Mon, 24 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanachama wa Chadema, jana walionyesha kutoridhika na kukasirishwa na sababu za kuahirishwa kesi ya wabunge 19 wa viti maalumu waliofukuzwa uanachama wa chama hicho.

Kesi hiyo iliahirishwa kwa madai kuwa shahidi ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Bara, Hawa Mwaifunga alifika mahakamani, lakini hakuweza kuendelea na ushahidi wake kutokana na kuugua.

Hivyo, Jaji Cyprian Mkeha anayeisikiliza aliiahirisha hadi Novemba 3, mwaka huu.

Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa Chadema nje ya Mahakama walisikika wakilalamika kuwa sababu iliyotolewa haina ukweli, bali ni mbinu ya kuchelewesha kesi ili waendelee kubakia bungeni, madai ambayo yaliungwa mkono na baadhi ya viongozi wa Bawacha.

Lakini kiongozi wa jopo mawakili wa wabunge hao, Ipilinga Panya alipinga madai hayo, akisisitiza kuwa mteja wake anaumwa na hata kwenda mahakamani jana walimshinikiza tu, “Hata Chadema wenyewe wanalifahamu tatizo lake.”

Walichokisema wanachama Chadema

Aliyekuwa mwenyekiti wa mpito Chadema Jimbo la Segerea, James Haule alisema hawezi kupinga kama kweli mtu anaumwa. “Hii inawezekana kuna suala la kuvuta muda tu, kwa sababu, ilipoahirishwa kesi Oktoba 13, waliomba itajwe Novemba 4, wakakataliwa. “Lakini leo imerudi ileile tarehe iliyokataliwa, hiyo ndio inatia mashaka kwamba huenda sababu ni ya kutungwa,” alisema.

Maoni hayo pia yameungwa mkono na Mwenyekiti wa Bawacha mkoani Tabora, Monica Ncharo aliyesema kuwa alivyomwangalia Mwaifunga hadhani kama ni mgonjwa.

“Sisi tumemkuta pale ni mzima anatembea, anaongea na wenzake. Sidhani kama ni sahihi kesi kama hii ikaahirishwa maana anaonekana ni mzima kabisa. Nadhani huo ni mchezo wa kuchelewesha muda ili waendelee kuwepo bungeni,” alisema Monica.

Naye Katibu wa Bawacha Mbeya, Lucy Ngondo alihoji kama anaumwa kwa nini alifika mahakamani hapo.

Wakili afafanua

Akijibu madai hayo, wakili Panya alisema kuwa mteja wake anaumwa kweli na alitaka asifike mahakamani bali atume tu barua na vyeti vya daktari. “Tulimwambia ni vema awepo, haitakuwa busara kwa Mahakama tuahirishe kwa barua na vyeti vya daktari. Tulikuwa kwenye kizimba kesi ni ya kwenu, tafadhali njoo iahirishwe ukiwepo. Na hata kesho atakuwa Aga Khan kwa ajili ya kuendelea na matibabu.”

Alisema kuwa tatizo hilo ni la muda mrefu tangu mwaka 2019, ambapo alilazwa juma zima katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya matibabu ya mgongo.

“Hata Chadema na hasa hao Bawacha wanalijua na hata viongozi wa Chadema wanajua huwa ana tatizo la mgongo na huwa hasafiri muda mrefu,” alisema wakili Panya. Alisema kuwa hata alipoitwa ofisini hapo alielezea na akamuuliza wakili Kibatala kama amesahau kuwa alilazwa hospitalini hapo wiki nzima wakawa wanakwenda kumuona, lakini Kibatala akacheka tu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live